Mashirika yanayotoa huduma za kiutu katika jamii hasa kwa kaya masikini na wanaoishi katika mazingira magumu yamekuwa mkombozi kwao kwa kuwapa misaada kutokana na baadhi kushindwa kumudu gharama za maisha.
Akizungumza katika hafla ya kugawa zawadi ya Krismasi kwenye Kanisa la Assembles of God Mazimbu kwa watoto na vijana mjini hapa, Dorcus Benjamin (24) amesema amekuwa akinufaika kwa kupata huduma mbalimbali ya baada ya kujifungua watoto pacha wawili na mzazi mwenzake kumtelekeza.
Dorcus amesema shirika la Compassion International Tanzania ni miongoni mwa mashiriki yanayosaidia jamii zinazoishi katika mazingira magumu na kaya masikini na kuwa mkombozi wa walengwa.
“Nikiwa na ujauzito wa watoto pacha nilitelekezwa na mwanaume aliyenipa ujauzito na watu wa Compassion walipata taarifa zangu na kuanza kutoa huduma ya lishe na matibabu hata baada ya watoto kuzawali wameendelea kutoa huduma, ”amesema Dorcus.
Amebainisha kuwa isingekuwa rahisi kwake kujipanga kulea mimba pekee yake na kukidhi mahitaji muhimu kama afya, chakula na mambo mengine katika kipindi cha ujauzito wake kutokana na aina ya maisha wanayoishi katika familia yao.
Mhumudu wa mama na mtoto na mawasiliano majumbani wa shirika hilo, Getruda Masubo amesema shirika hilo limeanzisha mpango wa kuhudumia wajawazito na wanaoishi katika mazingira duni.
Advertisement Katika hafla hiyo watoto na vijana 312 wanaoishi katika mazingira magumu na kaya masikini wamepatiwa msaada wa nguo kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi.
Mratibu wa shirika hilo, Lucas Kiluwasha amesema Compassion International Tanzania imetoa zawadi ya nguo kwa watoto hao kuanzia umri wa mwezi mmoja hadi miaka 22 zinazotoka kwa wafadhili wa shirika hilo.