Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Masasi alivyoona fursa katika kilimo cha viazi vyekundu

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakutaka kusubiri kuajiriwa licha ya kuwa na cheti cha elimu ya juu. Aliiona fursa na kuamua kuichangamkia haraka.

Huyu ndiye Edward Masasi mkulima wa zao la beetroot au kwa Kiswahili kiazi chekundu.

Anasema aliamua kuchangamkia fursa ya kilimo hicho baada ya kugundua kuwa zao hilo linahitajika mno hasa kwa watu wenye matatizo ya upungufu wa damu.

“Ukiona zao fulani, watu hawajishughulishi na kilimo chake, ujue hiyo ndio fursa ichukue. Hivi ndivyo nilivyoanza kilimo hiki,’’ anasema Masasi msomi wa masuala ya kilimo na utawala katika biashara.

Anaongeza:” Ukienda hospitali kama una tatizo la upungufu wa damu, unashauriwa ule mboga za majani na matunda na moja wapo ya matunda ambayo yanaongeza damu kwa wingi ni tunda la beetroot.”

Safari ndefu

Pia Soma

Mpaka alipofikia sasa, anasema haikuwa rahisi kufika hapo.

“ Nilivyomaliza chuo mwaka 2011, nchini India nilirudi nyumbani ambapo nilijua nitapata kazi nzuri yaani nitakuwa meneja katika ofisi fulani, lakini mambo yakawa tofauti, kwani kila nilipopeleka maombi ya kazi, sikupata kazi” anasema huku akitingisha kichwa.

Ni kwa sababu hiyo maisha hayakuwa rahisi kwake. Anakumbuka siku ambayo alilazimika kutembea kwa miguu kutoka Magomeni hadi Kibamba kwa kukosa nauli ya Sh400!

Masasi ambaye kwa sasa anamiliki kampuni ya kilimo anasema, katika harakati zake za kutafuta kazi, siku mmoja rafiki yake alimpigia simu na kumueleza kuwa kuna kampuni imetangaza nafasi za kazi hivyo watu wanatakiwa kwenda kwa ajili ya kufanya usaili.

“Siku hiyo niliamka asubuhi sana nikaanza kutembea kwa miguu kutoka Magomeni nilipokuwa nakaa kwa ndugu hadi Kibamba kwenda kufanya usaili,’’ anasema na kuongeza kuwa katika usaili huo hakufanikiwa kupata ajira.

Hapo ukawa mwanzo wa kufanya kazi za mbalimbali za vibarua.

“ Nilifanya pia kazi katika kampuni ya kusaga unga ambapo hapo nilikuwa nalipwa mshahara wa Sh 100,000 kwa mwezi, hivyo nikaanza kuweka akiba kidogo kidogo” anaeleza.

Aanza kulima betroot

Anasema alianza rasmi kulimo hicho mwaka 2017 kwa mtaji wa Sh 500,000 katika eneo la nusu ekari, lakini kwa sasa analima eneo la ekari moja, huku mtaji ukiongezeka na kufikia zaidi ya Sh 5milioni.

Kwa nini aliamua kulima zao hilo? Anasema: “Niliamua kulima kilimo cha beetroot kutokana na kuona fursa kubwa niliyoiona katika masoko yake kwa maana ni zao lililo na uhakika wa soko, kwani wakulima wake ni wachache na na huku mahitaji yakiwa makubwa,’’

Soko lake

Anasema wateja wake wakubwa katika zao hilo ni katika maeneo ya hoteli, maduka makubwa ya jumla(supermarkets) na masoko ya Kariakoo na Kisutu. Kwa saa anasema kilo moja ya zao hilo anauza kwa Sh 5000.

Pamoja na zao hilo kustawi zaidi katika maeneo ya ubaridi kama vile mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Masasi amekuwa akitoa mafunz ya kilimo hicho katika shamba darasa lililopo jijini Dar es Salaam eneo la Madale.

Anafafanua kuwa kilimo hicho kina stawi zaidi katika ardhi yenye udongo wa tifutifu na kichanga kiasi. Pia udongo wake unatakiwa kuwa na uchachu (ph) wa 5.8 ambapo hapo itamlazimu mkulima kufanya vipimo vya udongo kitaalamu katika maabara ili aweze kujiridhisha kabla ya kuamua kulima zao hilo.

Anasema zao hilo huchukua miezi mitatu tangu kupandwa hadi kukomaa na kuvunwa na kwamba mche unatumia muda siku 21 tangu unapopandwa katika kitalu hadi kuupeleka shambani kwa ajili ya kupandwa .

“ Beetroot baada ya kuvunwa mara ya kwanza inaweza tena kuvunwa mara tatu zaidi ndipo mkulima unaweza kuuondoa mche shambani” anasema.

Pamoja na changamoto za ugeni wa zao hilo kwa baadhi ya watu hali inayomlazimu awe anatoa elimu ya manufaa yake, Masasi anasema kilimo hicho kimemwezesha kuanzisha kampuni binafsi iitwayo Masasi Farming and Agro Business iliyopo Madale, jijini Dar es Salaam.

“ Kupitia kampuni yangu, naendelea kutoa elimu kwa wakulima wengine ili waweze kulima zao hili la kisasa na kUpata faida, lakini kizuri zaidi nimeweza kuongeza mashamba zaidi kwa ajili ya uwekezaji,’’ anaeleza.

Masasi anawashauri vijana wenzake kuingia kwenye miradi ya kilimo kwa kuunda vikundi.

‘’Kilimo sio lazima uanze na maeneo makubwa, hapana, hata katika eneo dogo unaweza kuendesha kilimo,’’ anasema na kuongeza:

“ Unaweza kukodisha shamba la nusu ekari na kulima zao unalotaka na kupata faida ambayo itakupeleka kuanza kuwekeza katika mashamba makubwa.’’

Chanzo: mwananchi.co.tz