Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mary Chipungahelo azikwa Dar, CCM yamsifu kwa ujasiri

0871856b23707e455c93e69aa46d792b.jpeg Mary Chipungahelo azikwa Dar, CCM yamsifu kwa ujasiri

Fri, 14 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba amewaongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mary Alice Chipungahelo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano wilayani Ilala.

Katika salamu zake za rambirambi, Kamba alimtaja kiongozi huyo ambaye alijulikana kwa jina la Mary Chipps, kuwa mwalimu katika sekta ya maadili na utumishi bora katika sekta ya ustawi wa jamii.

Alisema Mary Chipps alikuwa mwanamke jasiri aliyefanya kazi kwa kujiamini na katika ufanisi mkubwa kutokana na elimu aliyoipata wakati wa ukoloni. Alisema CCM itamkumbuka kutokana kuwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha African National Unio (TANU) mwaka 1954 na baadaye CCM mwaka 1977.

Balozi Mstaafu wa Tanzania katika mataifa mbalimbali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi Wastaafu Tanzania, Christopher Liundi alimwelezea Mary Chipps kuwa alikuwa kielelezo kizuri kwa wanawake nchini.

Alisema kutokana na Tanzania kuwa na wasomi wachache wakati huo, Chipps alikuwa mmoja kati ya wanawake wachache waliopata elimu enzi za ukoloni ndio maana alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mkuu wa Wilaya.

“Mama Chipps kwa hakika alikuwa hazina kubwa kwa taifa kwa sababu alikuwa mchapa kazi mzuri na mfano wa kuigwa katika utendaji kazi ndani ya serikali na katika chama kwa ujumla,” alisema Balozi Liundi.

Balozi Mstaafu Peter Kalaghe alisema katika utumishi wake, Mary Chipps alikuwa kiunganishi cha watumishi wa umma na wa sekta binafsi kutokana na utendaji kazi wake wa kuwafundisha watumishi wote bila kujali sekta atokayo.

Misa takatifu ya kumuombea Mary Chipps iliongozwa na Kasisi Kiongozi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano, John Mlekano, ambaye katika mahubiri yake aliwataka waumini wote kujiandaa na mauti kwa kujiweka karibu na Mungu.

“Binadamu wote tutarejea tulikotoka, kinachotakiwa ni kujiandaa mapema ili siku ikifika turejee kwa Mungu wetu tukiwa wasafi tusiokuwa na wasiwasi mbele za Mungu,” alisema Kasisi Mlekano.

Mary Chipungahelo alizaliwa mwaka 1933 wilayani Muheza mkoani Tanga na kupata elimu ya msingi darasa la kwanza hadi la nne mwaka 1940 hadi 1943 katika Shule ya Wasichana ya Uhuru, Dar es Salaam.

Alijiunga na elimu ya sekondari katika Sekondari ya Machame darasa la tano hadi la nane kuanzia mwaka 1944 hadi mwaka 1947. Aliendelea na elimu ya sekondari katika shule hiyo ya Wasichana ya Machame kuanzia mwaka 1948 hadi mwaka 1951 na baadaye alipata kozi ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Machame 1951 hadi 1954.

Alifanya kazi katika ngazi na taasisi mbalimbali ikiwamo Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Bwiru mwaka 1953 hadi 1959; alikuwa Katibu wa Kwanza wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Makao Makuu (1972-1976), na mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda alikohudumu hadi mwaka 1987.

Mwaka 1987 aliteuliwa kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa hadi mwaka 1990 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hadi mwaka 1993. Aliwahi kuteuliwa kuwa Mshauri wa Ubalozi wa Tanzania mjini Ottawa, Canada.

Mary Chipps alifunga ndoa na Dk Bernard Chipungahelo mwaka 1956 na kujaliwa kupata watoto sita; wa kiume wawili na wakike wanne. Ameacha watoto sita, wajukuu na vitukuu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz