Mwili wa kijana mmoja unaosadikika kuwa miongoni mwa miili mitano iliyopatikana eneo la Mlima Senjele wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe Mei 10 mwaka huu, umefukuliwa baada ya kutambuliwa kwa picha kisha kwenda kuzikwa kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Theopista Mallya amewaambia waandishi wa habari kuwa mwili huo ulizikwa na Serikali Mei 21 mwaka huu katika makaburi ya Mantengu wilayani Mbozi baada ya kutotambulika.
Amesema Marehemu ametambuliwa na mama yake aitwaye Irene Kivenule Xavery (40) mkazi wa Dodoma na mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya nje ya nchi na kumtaja Marehemu kuwa ni Feruzi Muna (25) ambaye alikuwa mfanyabiashata na mkazi wa jijini Dodoma.
"Mama huyo alifika kutuoni na kudai kupotelewa na mwanaye na ndipo aliomba kuutambua mwili huo kupitia picha zilizohifadhiwa kituo cha Polisi," amesema Mallya.
Kamanda Mallya amesema Juni 20, 2023 taratibu za kimahakama zilifanyika na kutolewa kibali cha kufukuliwa mwili wa marehemu kwa ajili ya kwenda kuzikwa nyumbani kwao Igowole Mufindi mkoani Iringa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la wahehe.
Mei mwaka huu miili ya watu watano wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 30 ilipatikana katika Mlima Senjele ikiwa imetupwa na baadaye Serikali kuizika baada ya kutotambulika.