Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Marealle ataka kaburi la mama yake mdogo lifukuliwe

101014 Pic+mareale+2 Marealle ataka kaburi la mama yake mdogo lifukuliwe

Sun, 5 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mfanyabiashara maarufu nchini, Frank Marealle, ameiomba mahakama, pamoja na mambo mengine, itoe amri ya kufukuliwa kwa kaburi la mama yake mdogo, Veronica Mlanga.

Frank, ambaye pia ni Mangi wa Wachaga wa Marangu, ameiomba mahakama itoe amri hiyo ili jeneza lenye mwili wa Veronica lifukuliwe na kwenda kuzikwa katika eneo halali la marehemu.

Mwili wa mwanamke huyo ambaye alikuwa mke wa sita wa Mangi Marealle II, ulizikwa Machi 21 katika kitongoji cha Moori, kijiji cha Lyamrakana. Polisi walisimamia mazishi hayo.

Siku tatu kabla ya mazishi hayo, wakili wake, Modestus Njau aliwasilisha ombi mahakamani kwa hati ya dharura, akiiomba itoe zuio ili asizikwe eneo hilo kwa kuwa ni eneo halali la Frank.

Hata hivyo, Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, halikutoa amri yoyote kuzuia maziko hayo na badala yake likatoa wito wa pande zote mbili kufika mahakamani ili zisikilizwe. Hiyo ilikuwa fursa kwa upande wa pili kuzika.

Lakini juzi, wakili huyo alifungua maombi mengine katika baraza hilo na kupewa namba 51 ya 2020. Sasa analiomba baraza litoe tamko kuwa eneo alikozikwa Veronica ni la Frank, mwili uliozikwa eneo hilo, ufukuliwe na kuzikwa eneo halali la marehemu linalojulikana kama Pata.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Katika kesi hiyo, mfanyabiashara huyo anaiomba mahakama imuamuru Acley Marealle kulipa pia gharama za shauri hilo na nyingine itakazoona zinafaa.

Frank anaeleza kuwa anamiliki kihalali ardhi hiyo tangu mwaka 1931 kupitia kwa mama yake aitwaye Asinath Marealle aliyekuwa miongoni mwa wake wa Mangi David Marealle.

Anasema mwaka 1961, baba yake aliwagawia mashamba watoto wake, akiwemo Dk Wilfred Marealle, ambaye wakati huo alikuwa amepata ufadhili kwenda kusoma nje ya nchi.

“Kutokana na sababu hiyo baba yetu alimgawia Dk Wilfred Marealle upande wa magharibi, upande wa kaskazini na eneo la kusini lilibaki wazi, lakini baadaye alipewa Veronica ambaye ni mama wa Acley,” anadai.

“Lakini kabla ya Machi 18, 2020, mjibu maombi (Acley) bila haki yoyote, aliingia kwa jinai eneo lake na kuchimba na kujenga kaburi kwa ajili ya kumzika mama yake, Veronica Mlang’a.”

Kutokana na kuumizwa na kitendo hicho, aliwasilisha maombi Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi na kupewa namba 76 ya 2020, lakini baraza hilo likashindwa kutoa zuio la mazishi kwa wakati mwafaka.

Kama haitoshi, aliwasilisha malalamiko kituo cha polisi cha Himo akimtuhumu kuingia eneo lake bila ya ruhusa, na hivyo kulitaka jeshi hilo kuzuia mazishi kufanyika eneo hilo na kwamba polisi waliahidi kuwazuia.

Hata hivyo, anaeleza, licha ya mkuu wa kituo hicho ambaye hakumtaja kwa jina kuahidi kuzuia maziko hayo, ni ofisa huyohuyo ambaye alishuhudia maziko hayo pasipo kumzuia mjibu maombi.

Frank amewasilisha orodha ya nyaraka 14 ambazo anategemea kuzitumia kuthibitisha uhalali wa eneo hilo, miongoni mwa nyaraka hizo ni muhtasari wa kikao cha halmashauri ya ukoo wa Marealle cha mwaka 1967.

Wakili Jullius Semali, anayemtetea Acley alipoulizwa jana, alikiri kutaarifiwa kuhusu uwepo wa shauri hilo lakini akasema asingeweza kuzungumza hadi pale atakapopata nyaraka na kushauriana na mteja wake.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa Aprili 6, 2020.

Chanzo: mwananchi.co.tz