Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mara wapongezwa kufufua zao la kahawa

86241c30d0468e2d42c586b66e8f7081 Mara wapongezwa kufufua zao la kahawa

Sun, 22 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeupongeza uongozi wa mkoa wa Mara kwa mkakati wake wa kufufua zao la kahawa sambamba na mazao ya pamba na mkonge ili kuwa na uhakika wa kipato kwa wakulima wake.

Pongezi hizo zimetolewa juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya aliyetembelea kituo maalumu cha mafunzo ya wakulima kwenye viwanja vya maonesho vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama .

" Naupongeza sana uongozi wa mkoa wa Mara kwa jitihada zake za kufufua mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa,pamba na mkonge kwani yana mchango mkubwa katika kumaliza umasikini wa wananchi wetu" alisema Kusaya.

Akiwa Butiama, Kusaya alipokea taarifa ya wilaya iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Anna Rose Nyamubi aliyesema wamepanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa kupanda miche 340,000 ili baada ya miaka mitatu wawe na uwezo wa kuvuna tani 1,000 za kahawa kutokana na hali ya hewa nzuri na utayari wa wakulima.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kusema kupitia kituo cha maonesho ya kilimo cha Mama Maria Nyerere, taasisi za umma na binafsi zimeweka mashamba darasa maalumu kufundisha wakulima namna sahihi ya kuzalisha mazao ya biashara ikiwemo kahawa, pamba, mkonge ,korosho na mazao ya chakula na mboga mboga.

Mkakati wa mkoa wa Mara ifikapo mwaka 2023 waongeze uzalishaji kahawa toka tani 1,800 za sasa hadi kufikia tani 15,000 kupitia uhamasishaji wakulima kuanzisha na kufufua mashamba .

" Butiama tulipaswa kuwa juu kwenye mafanikio ya kilimo kutokana na hali ya hewa nzuri,hivyo tunaomba wizara ya kilimo ishirikane nasi kuhamasisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao na pia kufufua skimu za umwagiliaji " alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Akijibu maombi hayo Katibu Mkuu Kusaya alisema kupitia taasisi za utafiti wa zao la kahawa (TACRI) taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) na Wakala wa Mbegu (ASA) atahakikisha wanafika mkoani Mara mapema kutoa elimu ,kuzalisha mbegu na kutoa matokeo ya tafiti za kusaidia mkulima kuinua tija na uzalishaji wa mazao.

Katika hatua nyingine Kusaya ameagiza Wakala wa Mbegu( ASA) kupeleka mbegu bora za mahindi na mazao mengine mkoani Mara na kuuza kwa bei ya shilingi 5,500 kwa mfuko wa kilo mbili ili wakulima wapande msimu huu wa mvua.

Katika kuhakikisha mkoa wa Mara unafanikiwa kufufua mazao ya kimkakati Kusaya ameagiza wataalamu wa mkoa kupanga maeneo maalumu ya kuzalisha mazao ya biashara badala ya ilivyo sasa kulima kila eneo au wilaya hali inayosababisha ugumu kwa wataalam kuwafika wakulima.

"Tusiwaache wakulima walime kilimo cha mazoea, tuwashauri kitaalamu na kuweka kanda ili wanufaike na utaalamu na kuwa tuwashauri wapime afya ya udongo kabla ya kulima ili wajue aina ya mazao na mbolea ya kutumia kwa lengo la kuwa na uhakika wa uzalishaji" alisema Kusaya.

Chanzo: habarileo.co.tz