Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapya yaibuka uthamini Bonde la Msimbazi

Bonde Mto Msimbazi.jpeg Mapya yaibuka uthamini Bonde la Msimbazi

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Siku chache baada ya serikali kutangaza kurudiwa kwa uthamini kwa watu wananchi wanaopaswa kupisha mradi wa uendelezaji bonde la mto Msimbazi, Wakazi wa Misheni Kota, Kata ya Mchikichini, wamelalamika eneo lao kutokuwepo katika orodha ya wanaopaswa kufanyiwa uthamini upya.

Bathelemeyo Chang'ambwe mmoja wa wakazi hao, amesema yeye ni miongoni mwa waliosaini fomu za kukubali kupisha mradi huo, na kwamba hakuridhika uthamini uliofanya hivyo akaandika barua ya malalamiko lakini anashangaa kwamba si miongoni mwa watakaofanyiwa uthamini upya.

"Serikali imesema tuliolalamika tutafanyiwa uthamini mpya, lakini katika tangazo ambalo serikali imelotoa la kuanza shughuli hiyo kesho, hatupo,” amesema mkazi huyo.

Ukiacha kutokuwepo katika orodha, mambo mengine ambayo waathirika wa mradi huo wanalalamikia ni kutoonana na mthamini mpya aliyepewa kazi ya kufanya shughuli hiyo.

Aisha Sariko, amesema: “Mfano mimi nina nyumba mbili eneo moja ambazo zote zina kila kitu ndani (self-contained), moja nakaa mwenyewe na ina vyumba viwili na vyumba viwili vya biashara ambayo nimeandikuwa fidia ya Sh23 milioni na nyingine nimepewa Sh24 milioni.”

"Nyumba hii inanisaidia kusomesha watoto wangu na wengine wanatarajia kwenda chuo mwaka huu, hivyo naziona ndoto zao zikiwa zinaenda kuzimika kwa shughuli hii ya uthamini, serikali ielewe kuwa hatuupingi mradi ila ni namna wanavyotuondoa hapa ndio haturidhiki," amesema Aisha.

Juliana Mtui, mkazi wa Msimbazi Bondeni, amesema ameishi hapo zaidi ya miaka 30 na usichana wake wote ametumia nguvu zake kujenga hapo.

"Pamoja na kutumia nguvu zangu hizi zote kwa miaka 30, leo tunaambiwa tunalipwa jengo tu kwa kile kilichodaiwa kuwa hili ni eneo hatarishi, kama eneo ni hatarishi kwa nini tulikuwa tukilipa kodi za majengo," amehoji Juliana.

Mwenyekiti kamati ya ufuatiliaji wa mitaa sita, Charles Swai, amesema wamekuwa wakipata wakati mgumu kutoka kwa wananchi hao kuwa wapo upande wa serikali kutokana na hatua iliyofikiwa kwamba hawajasikilizwa kilio chao.

Kutokana na hilo, Swai amesema wananchi hao wanawahamasisha waende wakafungue kesi mahakamani kama madai yao hayatafanyiwa kazi.

Seleman Cheyo, Mwenyekiti wa mradi walioathirika Msimbazi Bondeni, amesema tangazo linasema linaenda kuhakiki kwa mara ya pili na kundi lingine kusainishwa mkataba wa malipo.

"Huyo anayeenda kufanya shughuli hiyo kesho, hajaonana na sisi hadi leo, hivyo hatujui kama amefanyia kazi malalamiko yetu au la, angepaswa akutana na sisi kwanza," amesema Cheyo.

Akizungumzia suala hili Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ilala Kota, Amin Waziri amewaondoa wasiwasi wananchi na kueleza kuwa hakuna atakayeondoka eneo hilo bila kupata haki zake.

"Kinachoenda kufanyika kwenye uhakiki na uthamini ni katika kutafuta suluhu ya malalamiko ya waathirika kwani kuna makundi matatu katika sakata hilo ikiwemo waliokataa kabisa kusaini, waliokubali na waliokubali lakini wana malalamiko,"amesema Waziri.

Chanzo: mwanachidigital