Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapigano ya vijiji jirani Mara yamkera RC Mtambi

Ascdcdg Mapigano ya vijiji jirani Mara yamkera RC Mtambi

Wed, 15 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa huo kuwakamata watu wote waliohusika kwenye tukio lililosababisha watu wanne kujeruhiwa na nyumba kadhaa kubomolewa na zingine kuchomwa moto katika Kijiji cha Mekomariro Wilaya ya Bunda na Remng'orori wilayani Serengeti.

Tukio hilo lilitokea Mei 12, 2024 asubuhi baada ya watu wanaodaiwa kutoka Kijiji cha Mekomariro kuvamia Kijiji cha Remng'orori ambako waliwajeruhi baadhi ya watu kwa mishale na kubomoa nyumba kadhaa za wafugaji.

Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni mgogoro wa kugombea eneo la ardhi, ambalo lipo katikati ya vijiji hivyo, ambalo mara kwa mara limekuwa likizua mvutano.

Ardhi hiyo hutumika kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo.

Akizungumza katika Kijiji cha Remng'orori wilayani Serengeti leo Mei, 15, 2024 mkuu huyo wa mkoa amesama Serikali haitavumilia tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi.

"Wote waliohusika wakamatwe, nasikia wapo na wanasiasa, kila aliyehusika hata kama ni kiongozi wa Serikali akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema Mtambi.

Amesema Serikali hataki kuona mapigano hayo yakiendelea bali inataka kila Mwananchi aishi kwa amani katika kijiji chake.

Hata hivyo, amesema tayari hatua kadhaa zimeshachukuliwa dhidi ya mgogoro huo ikiwamo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

“Mgogoro wa hapa ulianza tangu mwaka 1954 na hutokea kwa sura tofauti, hivi karibuni aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara kabla yangu, alileta timu ya wataalamu na tayari wamefanya kazi yao tuko katika hatua ya kutekeleza yale waliyoyabaini sambamba na mapendekezo yao," amesema.

Mtambi ametoa onyo endapo mgogoro huo utaendelea, atalazimika kuchukua hatua kali zaidi, ikiwa ni pamoja na kulichukua eneo hilo linalogombewa na kulikabidhi kwa taasisi ya Serikali ili lipangiwe matumizi mengine.

Amesema Mkoa wa Mara una uhaba mkubwa wa ardhi kwa sababu asilimia 36 ya ardhi ya mkoa huo imechukuliwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na asilimia 36 zingine zimechukuliwa na Ziwa Victoria.

Amesema asilimia 28 pekee ya ardhi iliyobaki ndiyo inayotumika kwa makazi na shughuli zingine za kiuchumi, zinazofanywa na wanachi.

Pamoja na uhaba huo, Mtambi amesema asingependa kuona maeneo mengine zaidi yanatwaliwa na kukabidhiwa kwa taasisi za Serikali badala ya kutumiwa na wananchi.

"Narudia tena, tabia ya kujichukulia sheria mkononi ikome, wana Mara hebu tubadilike, tujielekeze kwenye mambo yanayoleta maendeleo, haya mambo ya kufanyiana ubabe na ukorofi hayana faida yoyote zaidi ya kuleta hasara,” ameonya mkuu huyo wa mkoa.

Pia amepiga marufuku tabia ya wafugaji kuharibu mashamba ya wakulima kwa makusudi, akiwataka wananchi ambao mashamba yao yataharibiwa kuanzia sasa, watoe taarifa mara moja kwa uongozi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Simulizi ya mgogoro

Wakieleza namna tukio la juzi lilivyotokea, baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wamesema chanzo ni mkazi wa kijiji cha Mekomariro aliyejulikana kwa jina la Magoto Maiga kufika katika eneo hilo la mgogoro kuchukua miti aliyokata siku iliyotangulia.

“Huyu mtu alikata miti kwa ajili ya ujenzi Jumamosi na Jumapili saa 12 asubuhi alifika pale alipoiacha ili aichukue, ghafla akazingirwa na vijana kutoka Kijiji cha Remng'orori wakawa wanamzuia asiichukue, ndiyo ugomvi ukaanza,” amesimulia Joseph Wambura, mkazi wa Mekomariro.

Amesema walipokuwa wanabishana kijana mmoja alimchoma na mshale Maiga naye akapiga kelele na watu kijijini wakajitokeza, yakazuka mapigano.

Mkazi wa Kijiji cha Remng'orori, Robert Kyariga amesema baada ya watu kutoka Mekomariro kufika kijijini kwao, walianza kuwashambulia wenzao wa kijiji hicho kabla ya Polisi kufika na kutuliza ghasia hizo.

Katika tukio hilo, watu wanne wakazi wa Kijiji cha Mekomariro walijeruhiwa kwa kuchomwa na mishale sehemu mbalimbali za miili yao na kwa sasa wanatibiwa katika Kituo cha Afya Mugeta wilayani Bunda.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vincent Naano amesema majeruhi watatu wanaendela vizuri na mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi.

Amewataja majeruhi kuwa ni Chacha Gibege, Magoto Maiga, Marwa Sira na Jona Faida ambaye amepelekwa Bugando kwa matibabu zaidi.

Chanzo: Mwananchi