Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapato, matumizi yawaponza viongozi wa mtaa Handeni

Sun, 20 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Wananchi wa mtaa wa Tuliani kata ya Kwediyamba halmashauri ya mji Handeni mkoani Tanga, wamemtaka mtendaji wa kata hiyo kuondoka na viongozi wote wa mtaa huo kwa kushindwa kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kwa zaidi ya mwaka mmoja. 

Wamesema hawaipokei taarifa ya mapato na matumizi waliyosomewa na uongozi wao ya Julai hadi Desemba, 2018 wakidai ina upungufu huku wakitaka waondolewe kwa kushindwa kuwasimamia kwani zipo taarifa za nyuma hawajasoma. 

Wakizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika jana Alhamisi Januari 17, 2019  walisema kuna mambo yanawafanya kutokubali mapato hayo kwa kuwa wanatajiwa kiasi cha fedha bila kupewa uchambuzi wake imepatikana vipi na kutumikaje. 

Mmoja wa wananchi hao, Shabani Msiwa alisema viongozi hao wanabadilishana madaraka bila kuwataarifu wananchi ambapo mtendaji wa mtaa wa sasa hawafahamu ameingia vipi hivyo kushindwa kuhoji baadhi ya vitu ikiwemo michango waliyochangishwa. 

"Huyu mtendaji sisi hatumfahamu, wala hakuna taarifa kuwa amekuja mtendaji mpya, taarifa yenu ya mapato na matumizi hatuipokei aje kuisoma yule mtendaji wa mara ya kwanza kuna maswali tunataka kumuuliza huyu hayafahamu majibu yake," alisema Msiwa. 

Mtendaji wa kata ya Kwediyamba, Hamza Madebe alisema kwa kuwa wananchi wameonyesha hofu kutokana na mapato yao atatafuta undani wake kwa kwenda kuangalia hesabu husika huku wakitafuta wananchi ambao watashirikishwa kupata ukweli wake. 

Kuhusu mtendaji wa zamani kuwa hajakabidhi ofisi hilo alikuwa halifahamu hivyo atafuatilia taratibu zilizofanyika kukabidhiana ofisi.

Diwani wa Kwediyamba, Salehe Sebo alisema mtendaji mpya wa mtaa kutokukabidhiwa ofisi na mwenzake aliyeondoka ni kosa kwani mtumishi anatakiwa kukabidhi ofisi ikiwemo nyaraka hivyo kama hajakabidhiwa atakuwa amefanya makosa. 

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Tuliani, Mohamedi Hoya alikiri kutosomwa taarifa ya mapato na matumizi kwa zaidi ya mihula miwili kutokana na kukosa mtendaji wa mtaa kwa muda mrefu.



Chanzo: mwananchi.co.tz