Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapato madogo Dar yamuumiza kichwa Makonda

9923 MAKONDA+PIC TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Unaweza kusema mkoa wa Dodoma kuongoza kwa mapato kati ya majiji sita yaliyopo nchini kumemtikisa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Paul Makonda.

Leo Ijumaa Agosti 3, 2018 Makonda amemtaka katibu tawala wa mkoa huo, Abubakar Kunenge kukutana na wakurugenzi wa halmashauri zote za jiji hilo kupitia taarifa za mapato ili kubaini sababu za Dar es Salaam kupitwa na Dodoma katika ukusanyaji wa mapato.

Ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuwakaribisha wakuu wa wilaya wapya na kuwaaga waliohamishwa vituo vya kazi.

Makonda amesema lazima wakurugenzi wa Dar es Salaam waongeze vyanzo vya mapato, kusimamia taarifa za mapato katika halmashauri zao.

"Haiingii akilini tumezidiwa na Dodoma kwenye ukusanyaji wa mapato, tutafanya kila namna kurejea katika nafasi yetu," amesema Makonda akimueleza Kunenge aliyechukua nafasi ya Theresia Mbando aliyehamishiwa mkoa wa Pwani.

Soma Zaidi:

Magufuli atoa maagizo mazito kwa Ma-RC

Makonda amemtaka katibu tawala huyo kuwa makini na taarifa anazopewa na wakuu wa idara kwa sababu wakati mwingine wanatoa taarifa za uongo.

“Nilishawahi kupewa taarifa saba za uongo na RAS, kwa hiyo uwe makini. Lazima uzipitie na kujiridhisha," amesema.

Pia, amemwagiza Kunenge kuanza na idara ya ardhi kwa sababu imeshindwa kufanya kazi zake na mkuu wa idara hiyo ni mzigo.

Amemtaka apange safu yake ya viongozi ili kuongeza ufanisi katika mkoa huo, akibainisha kuwa haridhishwi  na utendaji wao wa kazi katika kuwahudumia wananchi.

"Mpaka sasa nimetumia asilimia 37 ya nguvu zangu, asilimia 63 bado sijaitumia. Hilo linatokana na utendaji duni ndani ya mkoa wangu," amesema.

Kwa upande wake, Kunenge ameahidi kushirikiana na watendaji walio chini ya mkoa wake ili kuhakikisha wanafikia azma ya Makonda na Rais John Magufuli.

"Ninaahidi kushirikiana nanyi, kama una tatizo mfike ofisini kwangu lakini uwe na suluhisho kisha tunajadiliana," amesema Kunenge.

Juzi wakati akizungumza na wakuu wa mikoa baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Magufuli alisema kati ya majiji yote, Dodoma inaongoza kwa makusanyo ya  mapato ya Sh24.2bilioni ikiwa ni asilimia 123 ya makisio yao ya Sh19bilioni.

Amesema Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kongwe kuliko yote lilikusanya Sh15.3bilioni, Arusha (Sh10.3bilioni), Mwanza (Sh9.3bilioni), Tanga (Sh9.1bilioni) na Mbeya (Sh4.2bilioni).

Chanzo: mwananchi.co.tz