Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maofisa elimu kata kuwekwa darasani

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Maofisa elimu kata 330 kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wameanza kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo ya elimu endelevu kwa walimu kazini.

Mafunzo hayo ni katika kuhakikisha wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na pili wanakuwa na msingi mzuri wa kufahamu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK).

Akizungumza leo Jumanne Aprili 9, 2019 msimamizi na mratibu wa mafunzo hayo, Ibrahim Sungura amesema lengo ni waweze kuendesha na kuyasimamia mafunzo ya ualimu kazini kwa ajili ya kuwajengea uwezo na umahiri walimu wanaofundisha madarasa hayo.

Sungura amesema mafunzo hayo yamejikita katika ujenzi wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule wanazosimamia.

“Mafunzo yanalenga kuimarisha utendaji ni imani yangu tutaona mabadiliko chanya miongoni mwa maofisa elimu kata kwa kushirikiana na maofisa wengine watakaosimamia vyema mafunzo endelevu kwa walimu wanaofundisha darasa la kwanza na pili na wale wa awali,” amesema Sungura

Naye Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Mtwara, Abubakar Salehe amesema awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilianza Aprili 8 hadi 10 mwaka huu, ambayo ina washiriki 139 kutoka halmashauri za Lindi na awamu ya pili itaanza April 11 hadi 13 itahusisha washiriki 191  kutoka Mtwara.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Boniphace Ayubu amesema mfumo uliokuwapo haukuwa shirikishi na kutumia vitendo zaidi, lakini kutokana na mafunzo hayo yatawashirikisha wanafunzi kwa vitendo.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (Adem) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais (Tamisemi).



Chanzo: mwananchi.co.tz