Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manispaa Ubungo yapitisha bajeti ya Sh84bilioni mwaka 2019/20 lakini...

44121 Bonifaspic Manispaa Ubungo yapitisha bajeti ya Sh84bilioni mwaka 2019/20 lakini...

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ubungo,  Boniface Jacob amesema madiwani waligoma kutembelea miradi ya maendeleo baada ya kubaini hakuna mradi mpya uliofanyika licha ya bajeti ya mwaka 2018/19 kupitishwa.

Jacob ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 27, 2019 wakati akijibu maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,  Kisari Makori alipokuwa akifungua kikao cha  baraza la madiwani wa manispaa hiyo.

Jacob amesema kuna baadhi ya miradi inapingwa na madiwani  waligoma kuitembelea.

Amesema  baadhi ya miradi kutokaguliwa na kamati ya fedha ilitokana na matakwa ya kisheria kuweka wazi kuwa kila baada ya miezi mitatu kikao kinakaa kujadili mambo yaliyofanyika na kukuta hakuna hata mradi mmoja wa maendeleo uliokuwa ukifanyika mtaani.

Meya huyo amefafanua kuwa kusipokuwa na mradi mpya watendaji wanachomekea miradi viporo.

Amebainisha kuwa  madiwani walikaa kujadili kwa nini halmashauri haijatekeleza miradi ya maendeleo hata mmoja.

"Hakukuwa na mradi wa maendeleo uliotekelezwa hata mmoja kati ya miradi 110 kwa kata zote 15 na mitaa yote 97 ikiwamo ile iliyopitishwa kwenye bajeti iliyopita, madiwani wakaona hakuna haja ya kwenda kukagua na badala yake wakae wajadili kwa nini haifanyiki, na walilipwa posho kwa sababu walikaa siku nzima kujadili na wakatoa mwezi mmoja kwa watendaji kutaka majibu ya miradi hiyo" amesema Jacob.

Amesema kwa kawaida halmashauri inatakiwa ionyeshe miradi ya maendeleo iliyofanyika kwa miezi sita, badala yake ikaonyesha inayofanyika lakini haikuwa  kwenye bajeti.

Jacob amefafanua kuwa kuhusu kuwepo kwa mizengwe si kweli kwa sababu kwenye manispaa hiyo mbali ya mizengwe hata siasa za chama kwenye mambo ya maendeleo hakuna.

"Huku hakuna mizengwe wala siasa, wanaokuja kwako mkuu wa wilaya wanakuwa hawana maelezo sahihi ya wanachokisema, miradi ya maendeleo inasimaiwa ipasavyo," amesema.

"Umeona leo bajeti imepita bila kupingwa, kungekuwa na zengwe madiwani wangesubiri hapa wangeigomea bajeti."

Awali,  Makori amesema kuwa kamati ya fedha na uongozi iligoma kukagua miradi ya maendeleo na badala yake wakalipana posho.

Amesema kazi hizo ni kisheria sio za utashi, hivyo anashangaa mgomo huo wa kutokagua unatoka wapi.

Ameagiza suala hilo lifanyike mapema kabla ya kikao cha Baraza hilo kitakachofanyika  Machi, 2019  kitakachojadiri  taarifa za utendaji za kata.



Chanzo: mwananchi.co.tz