Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia ya watoto walivyowezeshwa kurudi shule Mara

4c8a212f7f17997c3d4dfa6f2e8426f2 Mamia ya watoto walivyowezeshwa kurudi shule Mara

Thu, 10 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ELIMU ni uhitaji muhimu na haki ya msingi kwa kila mtoto, lakini wakati mwingine baadhi ya watoto wamekuwa wakiikosa haki hiyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa kulitambua hilo na kwa kuzingatia kuwa elimu ni silaha muhimu ya kumkomboa mtoto kifikra, serikali licha ya kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya msingi mpaka kidato cha nne, ilianzisha programu ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) katika shule za msingi Tanzania bara.

Programu hiyo maalumu imegawanywa katika makundi makuu mawili; kundi rika la kwanza ambalo hujumuisha watoto walio na umri kati ya miaka 7 - 13 na kundi la pili ni wale walio na umri wa kati ya miaka 14 – 17

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), Tanzania bara mwaka huo ilikadiriwa kuwa na watoto zaidi ya milioni 3.5 waliopaswa kuwa shule za msingi lakini hawapo; kati yao watoto 1,968,910 walikuwa watoto wenye umri wa miaka 7 – 13 na 1,522,680 wenye kati ya miaka 14 – 17.

Ilielezwa kwamba watoto hao ama hawakuwa wameandikishwa shuleni kabisa au wameacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba, vifo, magonjwa na umasikini.

Zipo pia sababu nyingine nje ya ripoti hiyo zinazotajwa kuchangia watoto ama washindwe kuandikishwa shuleni ama kuacha shule ambazo ni pamoja na umbali kutoka nyumbani hadi shuleni, miundombinu na mazingira yasiyo rafiki hasa kwa walemavu na watoto wa kike, kukosa chakula shuleni, ukeketwaji, n.k.

Hata hivyo, mpango huu wa kuwanusuru watoto walio nje ya mfumo rasmi wa shule licha ya kusuasua kutokana na sababu kama hizo na nyinginezo, lakini baadhi ya matunda yake yamekuwa yakiendelea kuonekana kufuatia matokeo mazuri ya watoto hao kwenye mitihani ya upimaji ya darasa la nne na mitihani ya darasa la saba.

Mfano kwa upande wa mkoa wa Mara matokeo ya mitihani ya kujipima ya darasa la nne (2017 – 2019) na ile ya kuhitimu darasa la saba kwa kipindi cha miaka mitatu (2018 – 2020) inaonesha mafanikio makubwa katika mradi huo wa elimu kwa watoto walio nje ya mfumo rasmi wa shule.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Elimu wa Mkoa Mara, Ephraim Simbeye ni kwamba mwaka 2018 jumla ya wanafunzi 462 walio nje ya mfumo rasmi wa shule walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba katika wilaya zote tisa, kati yao 443 walifanya na waliofaulu walikuwa 257 sawa na asilimia 58 ya ufaulu.

2019 walisajiliwa 1,091, waliofanya walikuwa 957 waliofaulu ni 859 sawa na asilimia 89.8 ya ufaulu; mwaka huu 2020 waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba walikuwa 922, waliofanya 732 na waliofaulu ni 327 sawa na asilimia 44.7

Vivyo hivyo katika mitihani ya upimaji ya darasa la nne mwaka 2017 waliosajiliwa walikuwa 292, waliofanya 280 na waliofaulu ni 266 sawa na asilimia 91.1; mwaka uliofuata 2018 walisajiliwa 597, waliofanya 547 na waliofaulu 395 sawa na asilimia 72.2; na mwaka jana 2019 walisajiliwa 1169, wakafanya 1113, na wakafaulu 962 sawa na asilimia 82.3 ya ufaulu.

Mafanikio hayo hayakuja bure bali nyuma yake ipo serikali kupitia ofisi ya elimu mkoani Mara sanjari na wadau wengine wa elimu ikiwemo Mara Alliance (inayojumuisha pia madhehebu ya dini) chini ya ufadhili wa mfuko wa Graca Machel Trust (GMT), Educate a Child na Unicef.

Kwa mujibu wa meneja ufuatiliaji na tathmini wa mradi wa watoto walio nje ya mfumo wa shule kutoka Mara Alliance, Nollasko Mgimba; mkoa wa Mara una jumla ya vituo 430 vya kuwahudumia watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.

“Tuna jumla ya vituo 430 katika wilaya zote tisa mkoani hapa na hadi kufikia 2018 tulikuwa na jumla ya watoto 114,740 wenye umri kati ya miaka 7 – 17, kati yao 59,690 wana umri kati ya miaka 7 – 13 na wengine 55,050 wana umri wa kati ya miaka 14 – 17. Anasema Mgimba

Anasema chini ya mradi wa watoto walio nje ya mfumo wa shule mkoani Mara, katika awamu ya kwanza pekee wameweza kuwatambua watoto zaidi ya 20,000 wa umri wa kati ya miaka 7 – 17 na kufanikiwa kuwawezesha kuendelea na masomo yao kwa lengo la kuboresha maisha yao ya baadaye.

“Mbinu na mikakati ambayo tumekuwa tukitumia kuwabaini watoto hawa katika jamii ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara, kufanya vikao vya ushauri na watoto, wazazi na walezi ikiwemo kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba,” anasema Mgimba.

Anaongeza kuwa mbinu nyingine ambazo wamekuwa wakizitumia ni pamoja na kutumia matangazo na vipindi maalumu kupitia radio za kijamii, kuwatambua watoto, kuwathibitisha na kutunza taarifa zao.

Kuhusu malengo yao kwa awamu ya pili ya mradi huo meneja huyo anasema kuwa mikakati waliojiwekea ni pamoja na kuweka mtandao imara utakaowajengea uwezo walimu, bodi za shule na viongozi wa elimu kiwilaya kwa kutoa mafunzo na nyenzo sambamba na kuitia hamasa jamii.

Aidha kwa kupitia mradi huo ulio chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Mara Alliance chini ya ufadhili wa mfuko wa Graca Machel Trust wamekuwa wakiwapa mafunzo maalumu na mbinu za ufundishaji (walimu tarajali) vijana wa kike na kiume waliomaliza kidato cha nne na kisha kuwagawia vituo chini ya usimamizi wa walimu wenye taaluma kutoka serikalini.

“Lengo la mradi kwa awamu ya pili kwanza ni kuwawezesha watoto 40,000 wa mjini na vijijini mkoani Mara walio nje ya mfumo wa shule kupata elimu yenye ubora na pili ni kuzalisha walimu 430 na viongozi wa elimu kiwilaya 36 wenye ujuzi wa kutoa elimu ya msingi yenye ubora,” anasema Mgimba.w

Akizungumza hivi karibuni kwenye kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani ambayo huadhimishwa Novemba 20 ya kila mwaka, Askofu George M.M.M. Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma amezitaka taasisi na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kuiga mfano wa Graca Machel Trust.

“Mama huyu aliziona changamoto hizi kwa watoto kuacha masomo mkoani petu akalazimika kukubali ombi hili la kanisa kwa kutoa ufadhili wa hari na mali ili kufanikisha ndoto za watoto wetu,” anasema Askofu Msongazila aliyefanikisha kwa kiasi kikubwa kumshawishi mama Graca kuufadhili mradi huo.

“Elimu humbadilisha mtu na hasa akikubali kusoma na siyo kwenda shule.”

Chanzo: habarileo.co.tz