Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia ya wananchi Kagera kwenda kumzika JPM Chato

F226339e62c23f5a6a43e3b11f0e7db4 Mamia ya wananchi Kagera kwenda kumzika JPM Chato

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANANCHI wa halmashauri nane za mkoa wa Kagera wataanza safari ya kwenda Chato kutoka maeneo yao kwa maandamano ya magari ili kushiriki kuaga mwili wa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kabla ya maziko yake yatakayofanyika kesho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, Hamimu Mahmoud jana alisema tayari makundi mbalimbali ya wanachama na wasio wanachama wa chama hicho wamejiorodhesha kufanya maandamano ya heshimu kutoka mkoa wa Kagera kwa safari ya usiku ili kuungana na ndugu zao wa Chato kwenye msiba huo.

Alisema Magufuli alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Kagera wakati akiwa waziri na mbunge wa Biharamulo Mashariki kabla ya jimbo hilo kuwa Chato na kuhamishiwa katika mkoa wa Geita .

Alisema Magufuli pia alikuwa mwekezaji mkubwa katika mkoa wa Kagera kwenye sekta ya mifugo kwenye Rachi ya Taifa.

Alisema matarajio ya wananchi wengi yalikuwa ni kuwa baada ya utawala wake angekuwa miongoni mwa wakazi wa mkoa huo.

Akizungumzia utekelezaji za ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, Mahamoud alisema Ilani hiyo ilitekelezwa kwa asilimia 90 katika miradi yote iliyokuwa imeorodheshwa mkoani humo.

"Ujenzi wa hospitali tatu za wilaya katika mkoa wa Kagera katika wilaya za Karagwe, Kyerwa na Halmashauri ya Bukoba, ujenzi wa barabara za lami, usafiri majini, elimu bure, ujenzi wa shule za msingi na sekondari, umeme vijijini kwa asilimia 75, urejeshaji wa nidhamu na mapambano dhidi ya rushwa ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kwa kasi kubwa ," alisema.

Mahmoud amewaondoa hofu wananchi ambao wanadhani miradi inayotelekezwa itasuasua baada ya kifo cha Magufuli, akisema CCM imewaandaa viongozi mahiri na kuandaa Ilani kama mwongozo muhimu wa utekelezaji, hivyo watarajie ikitekelezwa kwa kasi ileile na Rais Samia Suluhu Hassan.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili ulibaini kuwa, katika stendi kuu ya mabasi Bukoba kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi wanaokata tiketi za kwenda Chato.

Magari yanayokwenda Mwanza kupitia kwa mawakala wao walisema tangu juzi magari ya kwenda Chato yamekuwa yakijaa abiria kuliko kawaida.

Wakala wa mabasi ya Bunda express, Juma Mohamed alisema huenda magari ambayo yalikuwa yakifanya safari zake mchana wa saa 7:00 wakabadili na kwenda asubuhi Chato kwa sababu abiria ni wengi na wote wana lengo la kutaka kuaga mwili wa mpendwa wao.

"Abiria wengi wanasema wanataka walau washuhudie hata sanduku ili waamini kama kweli amekufa," alisema Mohamed.

Alisema mawakala wa mabasi watamkumbuka Magufuli kwa kuongeza ulinzi katika sehemu hatarishi barabarani na kudhibiti utekaji uliokuwa ukiwakumba wanachi na wafanyabiashara katika pori la Biharamulo, kuweka usawa kati ya tajiri na masikini na kuondoa kero katika maeneo ya stendi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz