Korogwe. Mamia ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani na waliotoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali wamekwama tangu jana mchana Ijumaa Oktoba 25, 2019 wilayani Korogwe na Handeni Mkoa wa Tanga.
Wamekwama kutokana na maji kupita juu ya daraja la Mandera na kulisomba daraja la Handeni mkoani humo.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Oktoba 26, 2019, Jane Mathias na Juma Kombo wamesema tangu jana saa 5 asubuhi wamekwama katika daraja hilo kutokana na wingi wa maji uliotokana na mvua inayoendelea kunyesha mkoani Tanga.
"Tumefika hapa jana saa 5 asubuhi hadi muda huu (leo saa1 asubuhi) hatuoni uwezekano wa kuvuka," amesema Mathias.
Kombo ameiomba Serikali kuondoa adha hiyo kwa sababu kwa wiki mbili sasa daraja la Mandera limekuwa likijaa maji.
"Ni aibu barabara muhimu kama hii watu kukwama kutokana na daraja kujaa maji, kila siku wanajenga vivuko hawaimarishi barabara," amesema Mathias.
Pia Soma
- Profesa Kabudi azitaja Uingereza na Marekani vikwazo dhidi ya Zimbabwe
- Mahakama yakataa kubadili jina la Mwanyika
- Pyramids watua, wawataja Tshishimbi, Balinya
"Hii barabara ilikuwa nzuri ila ukarabati uliofanywa hivi karibuni ndio umeongeza tatizo" amesema Mposi.
Akizungumza na Mwananchi asubuhi hii, kuhusu athari zilizotokea hadi sasa ikiwamo vifo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Mwangoka amesema maafa lazima yatakuwapo kwa sababu mvua inayoendelea kunyesha ni kubwa sana.
“Hali ya sasa maji yanapungua eneo la Mandera liliko Daraja la Mandera lakini bado hakupitiki,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.