Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia wamzika mwandishi wa habari wa MCL

14663 MCL+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Vilio na majonzi jana vilitawala wakati wa kuaga mwili wa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Raymond Kaminyoge.

Mwili wa Kaminyoge uliagwa jana nyumbani kwa dada yake Matilda katika Mtaa wa Maendeleo Kata ya Iyunga na kuzikwa katika Makaburi ya Lumbila Iwambi jijini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Akizungumza katika mazishi hayo, Mwinjilisti Dickson Mbwaga wa Kanisa la Moravian, Usharika wa Lumbila, aliwataka waumini kumrudia Mungu, “Vijana, Wakristo tumieni fursa za makanisa mengi yaliyopo Mbeya mkatubu.”

Mbwaga aliwataka waumini wa dini zote kumwombea marehemu Kaminyonge.

Awali, Mwenyekiti wa Mtaa wa Maendeleo, Elias Mwakyusa aliipongeza MCL kwa jinsi ilivyojitoa katika ugonjwa hadi mazishi.

Mwakyusa alisema msiba huo umeonyesha ni jinsi gani Kaminyoge alivyoishi vizuri na uongozi wa Mwananchi na kuomba ushirikiano huo uendelezwe katika jamii.

“Huu ni mfano wa kuigwa na inaonyesha ni jinsi gani alivyokuwa karibu na wafanyakazi wenzake na waajiri wake, kimsingi wananchi na viongozi wa eneo hili tunashukuru kwa mchango mkubwa uliotolewa na ushiriki wenu (MCL),” alisema.

Meneja Mauzo na Uendeshaji wa MCL, Arnold Kimanganu alisema, “Kaminyoge alikuwa ni mwandishi mzuri wa masuala ya uchumi, siasa, afya na mambo ya kijamii. Alikuwa ni kijana anayejituma na kushirikiana na wenzake.”

Marehemu Kaminyoge ambaye ameacha mke na watoto watatu, alifariki dunia juzi alfajiri katika Hospitali ya Rufaa Mbeya alikokuwa amelazwa.

Kaminyoge alizaliwa Julai 25, 1968 Iyunga, Mbeya na kupata elimu ya msingi wilayani Mufindi na mwaka 1986 alijiunga na Shule ya Sekondari Mpechi, Njombe ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1989.

Alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1996 katika kampuni ya The Guardian Limited na mwaka 2012 alijiunga na MCL.

Chanzo: mwananchi.co.tz