Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia wamzika aliyeuawa kwenye mazingira ya kutatanisha

85900 Pic+mamia Mamia wamzika aliyeuawa kwenye mazingira ya kutatanisha

Tue, 26 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hanang'. Mamia ya wakazi wa Mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang' Mkoani Manyara, wamejitokeza kwa wingi kumzika mkazi wa jijini Arusha, Sirili John anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Wakizungumza leo Jumatatu Novemba 25 kwenye kitongoji cha Lamai, Kata ya Katesh, wakazi hao wameiomba Serikali kufanya uchunguzi juu ya kifo hicho.

Mmoja kati ya wakazi hao, Ezekiel Bura amesema kifo hicho ni cha kikatili hivyo Serikali ichunguze kwa sababu kinahusisha mambo ya kisiasa.

Baba mzazi wa marehemu huyo, John Omary amesema hana imani na taarifa iliyotolewa na polisi juu ya mazingira ya kifo cha mtoto wake.

Amesema amepata taarifa kuwa askari polisi wanadai kuwa kuna uwezekano Sirili alijiua mwenyewe wakati mazingira ya tukio hilo yanaonyesha kuwa aliuawa.

Diwani wa Katesh, Peter Lowri ambaye msiba ulikuwa kwenye kitongoji cha eneo lake la Lamai amesema Sirili ameuawa kikatili.

“Nilikagua mwili wake na kukuta ameuawa kikatili, nadhani alipigwa na shoka kwenye mabega yote mawili na kifuani, ni kifo cha kikatili kweli kweli,” amesema Lowry.

Jirani wa eneo hilo, Yusuph Gong amesema waliishi miaka mingi kwenye kitongoji cha Lamai na Sirili kabla hajahamia jijini Arusha.

Gong amesema hajui mazingira ya kifo hicho ila alisikia Sirili aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali.

Katekista wa kanisa katoliki Katesh aliyeendesha ibada hiyo Victoria Charles amewaasa waumini walioshiriki ibada hiyo ya mazishi kutowazia kulipa kisasi kwa jambo lolote lile maishani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, amesema bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho.

“Hao wanaohusisha hicho kifo na masuala ya kisiasa wana lao jambo, tumefuatilia kata ya Unga Ltd marehemu Sirili hakuwahi kuchukua fomu ya kugombea lolote kupitia chama chochote,”  amesema kamanda Shana.

Marehemu Sirili ambaye alizaliwa Desemba 10, 1998 kwenye Kata ya Katesh na kufariki jijini Arusha, Novemba 21, hajaacha mke wala mtoto.

Chanzo: mwananchi.co.tz