Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia wamuaga mwalimu aliyekufa akimuaga JPM

RIP PIC Mamia wamuaga mwalimu aliyekufa akimuaga JPM

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMIA ya waombolezaji wameuaga mwili wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Viwegi, Jane Ngonde aliyefariki dunia wakati maelfu ya wananchi wakiuaga mwili wa Dk John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ibada ya kumuaga Jane ilifanyika katika Shule ya Msingi Viwegi iliyoko Chanika wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam.

Iliongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Menonnite Tanzania Jimbo la Ukonga, Abunel Mathube.

Mchungaji Mathube aliwataka waombolezaji waishi maisha ya imani, unyenyekevu na uwajibikaji kama alivyoishi Jane. Mwili wa Jane umesafirishwa kwenda Musoma mkoani Mara kwa maziko.

Jane ni kati ya watu waliopoteza maisha Machi 21, mwaka huu wakati wa kumuaga Dk Magufuli na inadaiwa kuwa kifo chake kilisababishwa na kukosa hewa kutokana na msongamano wa watu.

Alizaliwa Oktoba 8, 1979 katika mji wa Katoke wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Alipata Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu Dar es Salaam mwaka 2014 na mwaka 2017 alitunukiwa Shahada ya Uzamili. Mwaka 2020 aliteuliwa kuwa Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Viwege.

Hadi wakati anaaga dunia alikuwa Mzee wa Kanisa la Menonite na pia alikuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Pugu –Viwege. Ameacha mume Masenza Ngonde na watoto wanne; Francis (12), Florence (10), Raphael (6) na Fredrick (3).

Chanzo: www.habarileo.co.tz