Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mameneja Ruwasa watakiwa vijijini

E9592edcf05985f20f020b6fc33fecd2 Mameneja Ruwasa watakiwa vijijini

Mon, 5 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMENEJA wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wametakiwa kwenda vijijini kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchangiaji huduma za maji kwa mujibu wa Sheria ya Maji namba 5 ya mwaka 2019.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na kubaini changamoto zake wilayani Muheza.

“Kutokana na ziara yangu nimegundua wananchi wengi hawana uelewa juu ya sheria hii hasa katika suala la uchangiaji wa huduma za maji, haiwezekani kwa mwezi mtu analipa Sh 500 tu, mameneja Ruwasa nendeni kwenye miradi ya maji vijijini mkawaelimishe wananchi,” alisema.

Katika ziara yake hiyo, Nkanyemka aliyeambatana na maofisa kutoka Bonde la Mto Pangani, Mtaalamu wa Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji na Meneja Ruwasa mkoa wa Tanga, Upendo Lugongo, ambapo pia walitembelea miradi ya maji katika wilaya za Korogwe na Lushoto, pamoja na kukagua chanzo cha maji cha Bonde la Mto Zigi.

Wilayani Korogwe alitembelea mradi wa maji wa Mtonga-Msambiazi ambao unatoa huduma za maji katika vijiji vya Mtonga, Majengo na Msambiazi, ukiwa na thamani ya Sh milioni 595.

Changamoto aliyoikuta katika mradi huo ni maji kutolewa kwa mgao kutokana pampu kubwa iliyofungwa kwa ajili ya kusukumia maji kutoanza kufanyakazi kwasababu Shirika la Umeme (Tanesco) wilayani humo haijafunga mita kubwa ya kuiwezesha pampu kufanya kazi.

Aidha, alitembelea kituo cha maji katika kijiji cha Msambiazi ambacho kinapata maji kupitia mradi huo na kukutana na malalamiko ya wananchi kuwa maji hayo yana rangi na kuhofia kuyatumia kwa ajili ya kunywa na kupikia, badala yake wameamua kuyatumia kwa shughuli nyingine za nyumbani.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Nkanyemka alimuagiza Meneja Ruwasa Wilaya ya Korogwe, Sifael Masawe, kuhakikisha Tanesco inafunga mita hiyo ili kuondoa kero ya mgao wa maji pamoja na kuwatoa wananchi hofu kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Alisema serikali itahakikisha kupitia wataalamu wa Wizara ya Maji wanaondoa rangi kwenye maji hayo.

“Kupitia mradi mkubwa wa maji wa HTM ambao utatoa huduma za maji katika wilaya za Muheza, Handeni, Korogwe na Pangani kutoka chanzo cha Mto Pangani ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza Novemba mwaka huu, kutawekwa mtambo wa kuchuja maji hivyo hali hii haitajitokeza tena, serikali haiwezi kuwaletea maji yasiyo salama, yaliyopo ni salama tatizo ni rangi tu lakini yamepitia hatua mbalimbali za kuyachuja,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz