Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yaliyotikisa Rombo tangu mwaka 2003

63888 Rombopic

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kukiwa na habari yoyote inayoitaja Wilaya ya Rombo siku hizi, kila mtu anatamani kujua kuna nini. Hiyo inatokana na matukio kadhaa yaliyowahi kutikisa eneo hilo la Mkoa wa Kilimanjaro.

Mambo makubwa yanayokumbukwa zaidi ni manne ingawa tukio lililovuma zaidi ni lile lililoripotiwa kuwa baadhi ya wanaume wa wilaya hiyo hawana nguvu za kufanya tendo la ndoa kutokana na kuathiriwa na ulevi.

Habari hiyo iliyosambaa kama moto wa nyika, iliibuliwa mwaka 2015 na mkuu wa wilaya wa wakati huo, Lembris Kivuyo na kilichoifanya kuwa na mvuto wa aina yake ni madai kwamba baadhi ya wanawake walioko kwenye ndoa waliamua kwenda Kenya kukodi wanaume.

Eneo ambalo lilidaiwa kuathirika zaidi na unywaji wa pombe ya gongo na nyingine za kienyeji ni Kikelelwa lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.

Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo akitoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza la madiwani la halmashauri na kutaja Kikelelwa kama eneo linalohitaji jicho la pekee.

“Imefikia mahali baadhi ya wanaume wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya tendo hilo,” alisema Kipuyo.

Pia Soma

Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni iliyofanyika Mei 2015 ya kukamata pombe ya gongo katika eneo hilo la Kikelelwa.

Hata hivyo, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akisema si sahihi kuwajumuisha wanaume wote na ulevi huo au wanawake wote na kukosa tendo la ndoa.

“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida hiyo. Si sahihi kutoa kauli ya jumla,” alilalamika.

“Haiwezekani mtu mmoja aliyehojiwa akawakilisha wanaume au wanawake wenye matatizo hayo. Kauli hiyo imewadhalilisha wanaume na wanawake ambao hawahusiki na tatizo hilo,” alisisitiza.

Lakini pamoja na Selasini kutoa ufafanuzi huo, suala hilo liliendelea kutikisa mitandao ya kijamii huku katuni zikichorwa kuonyesha wanawake wakiwa wamebeba wanaume kutoka Kenya.

Matukio ya unywaji wa pombe kupindukia, yanaendelea kuitikisa wilaya hiyo hadi sasa na kuilazimisha Serikali kuanzisha faini ya Sh50,000 kwa atakayekutwa akinywa pombe saa za kazi.

Pamoja na tukio hilo, yapo matukio mengine yaliyoendelea kutikisa wilaya hiyo kabla na baada ya tukio hilo la ulevi wa kupindukia kwa baadhi ya wanaume.

Mauaji ya ajabu

Novemba 20, 2003, mkazi wa Kijiji cha Kamanga, Tumaini Ikera alishtakiwa kwa kumuua baba yake mzazi kwa kumchinja na kuzika kiwiliwili katika Msitu wa Rongani na kuuza kichwa chake Kenya kwa Sh300,000.

Katika hukumu yake aliyoitoa Aprili 6, 2009, Jaji Lawrence Mchome alimhukumu Tumaini adhabu ya kunyongwa hadi kufa huku akimuachia huru mshtakiwa wa pili, Laizer Kironyo.

Hata hivyo, Ikera hakuridhika na adhabu hiyo na kupitia kwa wakili wake, John Materu alikata rufaa akidai jaji alikosea kuyakubali maelezo yake ya ungamo kama kielelezo katika kesi hiyo.

Jopo la Majaji watatu lililoketi Arusha 2012, lilibariki hukumu hiyo na kueleza kuwa hata bila maelezo ya ungamo, kitendo cha mshtakiwa kuwapeleka ndugu na polisi alipozika kiwiliwili ilitosha.

Mwaka huohuo, mkazi mwingine wa Tarakea, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua msichana mwenye umri wa miaka 12 kwa kumbaka, akisema alitembelewa na ibilisi.

Ni katika kipindi hichohicho, mkazi mwingine wa Mahida Nduduni alipohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kumbaka mtoto wake wa kumzaa hadi kufa na kutumbukiza mwili chooni.

Mbali na hukumu hizo, matukio ya mauaji yameendelea kuitikisa wilaya hiyo na Machi mwaka huu, mwanamke mmoja mkazi Kijiji cha Lesoroma anadaiwa kuuawa na wanawake wenzake watano.

Kisa cha mauaji hayo kinadaiwa kilitokana na mtoto wa mwanamke huyo anayesoma darasa la sita kuiba chakula aina ya Ngararimo na kukila kutokana na kushikwa na njaa.

Juni 17 mwaka huu katika eneo la Samanga, mwanamke mwingine Emma Langoye (21) mwenye mtoto mchanga wa miezi 10, aliuawa kwa kuchomwa visu na mwili wake kutupwa barabarani.

Akutwa amekufa amepiga magoti na rozari

Moja ya tukio la nadra ni lile lililogusa imani ya dini ambako mwili wa kijana mwenye umri wa miaka 25 ulipatikana msituni. Kijana huyo alikuwa amekufa huku akiwa amepiga magoti, akiwa na bibilia na rozari shingoni.

Tukio hilo linalomhusu Godwin Massawe, mkazi wa Kijiji cha Msaranga, Kata ya Kisale, liimeibua hisia tofauti huku waumini wa Kikristo wakiamini kuwa kwa namna alivyokufa, ameenda mbinguni.

Vyanzo mbalimbali vilieleza kuwa kijana huyo baada ya kutoka ibada ya Jumapili Januari 20 mwaka huu hakurudi nyumbani mpaka alipokutwa Machi Mosi akiwa katika msitu huo.

Imani za ushirikina

Matukio ya ushirikina nayo yanadaiwa kuitikisa baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wanaoamini uwepo wa nguvu za giza. Baadhi wameenda mbali na kudai ndugu zao kufufuliwa.

Mwaka 2017, mkazi wa Kijiji cha Kiyongoni Usseri anayedaiwa kuuawa Desemba 27, 2017 na kuzikwa Desemba 31,2017 alidaiwa kuonekana akiwa hai mjini Moshi, tukio lililoibua gumzo Rombo.

Jambo lililoibua hisia zaidi ni pale wazazi wake walipothibitisha kuwa mtoto waliyemuona ndio huyohuyo waliyemzika miezi mitatu iiliyopita, lakini wakakataa kueleza mahali alipo kwa wakati huo.

Mwaka huo pia kulisambaa taarifa za kuwapo biashara ya viungo vya binadamu wilayani humo huku ikidaiwa kuwa kichwa kinauzwa kwa Sh5 milioni, taarifa ambazo zilikanushwa vikali na Serikali.

Chanzo: mwananchi.co.tz