Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo mawili Tanzania kufikia uchumi wa kati yatajwa

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizo katika nafasi nzuri barani Afrika kufika uchumi wa kati endapo juhudi zaidi zitawekwa.

Juhudi hizo ni uboreshaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo na masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo.

Hayo yameelezwa na rais wa Shirika la Kilimo barani Afrika (AGRA), Dk Agnes Kilibata alipokuwa akizungumzia mchango wa kilimo katika mkutano uliokutanisha wadau mbalimbali wa kilimo kutoka nchi 11 barani Afrika uliofanyika mkoani Iringa.

Dk Kilibata amesema  kilimo bado kina nafasi kuleta mageuzi ya uchumi Tanzania, kwamba kinachotakiwa kuongezwa ni upatikanaji mzuri wa mbegu, pembejeo na masoko ya mazao.

"Ninaomba wawakilishi wa AGRA kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, pembejeo bora na upatikanaji wa masoko ya uhakika,” amesema.

Mwenyekiti  kamati ya Bunge ya Kilimo na Mifugo, Mahamoud Mgimwa amesema asilimia  65 ya Watanzania wanategemea kilimo, ni jukumu lao kuhakikisha wanapata pembejeo za kutosha ili waweze kupiga hatua kiuchumi.

Pia Soma

Mgimwa amesema nchi imekusudia kwenda katika uchumi wa viwanda, ni vyema kujiimarisha katika sekta ya kilimo kuhakikisha asilimia 80 ya rasilimali ya viwanda inatokana na kilimo.

"Serikali itahakikisha inaboresha sekta ya kilimo katika kila eneo ili zipatikane pembejeo, mbegu bora kwa wakati vyenye bei nafuu, ni jukumu letu wabunge na kama Serikali kuhakikisha tunaondoa masharti ambayo yanawaumiza wakulima," amesema Mgimwa

Mwakilishi wa AGRA Tanzania, Vianey Rweyendela amesema shirika hilo limekusudia kugeuza maisha ya wakulima na jamii.

"Tumepata ugeni wa nchi 11 ambao wamekuja kujifunza kilimo nchini kwetu na utekelezaji wa kilimo ambao AGRA unafanya, tunawafundisha wakulima wetu kuanzia sokoni kuangalia mnunuzi ana changamoto gani au anahitaji zao gani kwa kiasi gani ndio waende shambani kulima kukwepa mazao kukosa soko,” amesema Rweyendela.

Chanzo: mwananchi.co.tz