Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama wa waziri agoma kuacha kazi ya mamalishe

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. “Naachaje biashara ya mamalishe wakati mwanangu ni waziri?” Hilo ni swali, lakini ndani yake limebeba ujumbe mzito kutoka kwa Fatma Omari Masanga, mama mzazi wa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Katika mahojiano na Mwananchi, Fatma (55), mkazi wa Bweni mkoani Tanga anaeleza jinsi anavyonufaika na biashara hiyo na asivyofikiria kuiacha kwa sababu ya nafasi aliyo nayo mwanaye serikalini.

“Shughuli zangu ni mamalishe, napika chakula, nakaanga maandazi, vitumbua, kuku, (lakini pia) nafuma vitambaa, mashuka na kupamba, nimefanya shughuli hizi tangu mwaka 1985,” anasema mama huyo ambaye mwanaye pia ni mbunge wa Pangani.

Tofauti na wazazi wengine wanapoona wanao wamepata nafasi za juu za madaraka huamua kupumzika kufanya shughuli wanazofanya, hasa zikiwa zile zenye kipato kidogo, Fatma anasema hilo halitatokea kwake.

“Naachaje biashara ya mamalishe wakati nimeiendesha kwa miaka 34 na ndiyo iliyosababisha Jumaa achaguliwe kuwa mbunge,” anasema.

“Wapiga kura waliwaacha wagombea wengine wenye uwezo wa kifedha na uzoefu mkubwa wakamchagua Jumaa kwa sababu kwanza ni mtoto wa mamalishe, lakini kubwa zaidi walisema hata wakimtafuta na kumkosa watakuja hapa kwa mimi mama yake ..na ndivyo wanavyofanya.”

Mama huyo wa watoto tisa anasema amekuwa kama katibu wa mbunge (mwanaye) kwa kuwa amekuwa ndiye mpokea kero wake mkuu kutokana na wananchi wengi kufika kwake wanapomkosa mwanaye.

“Sasa nikisema anijengee nyumba ya geti kali ili niondoke hapa, je hawa wananchi watakimbilia wapi? Si watasema tumempa ubunge na mama yake kamhamisha,” anasema. “Siyo Jumaa tu hata dada yake amejenga nyumba kubwa kule Pangani Mashariki ambayo kama ningetaka ningeweza kuhamia kule, lakini sijataka.”

Kwa nini hataki amsaidie?

Fatma anasema kuna siku alichukua simu ya mwanaye na kukumbana na ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa watu mbalimbali wakimuomba fedha, ambazo zilikuwa nyingi kuliko mshahara anaoupata.

“Nilimuonea huruma sana, kwa hali hiyo mimi kama mama sitakiwi kuwa kero, ni lazima nimwache afanye shughuli za wananchi pamoja na kwamba katika kipindi kifupi amefanya mengi lakini suala la barabara bado linawasumbua wana-Pangani,” anasema.

Mzazi huyo anasema, “sababu nyingine ya kuendelea kuwa mamalishe ni kwamba nataka kuwajenga wadogo zake Jumaa kuwa wajasiriamali na siyo wategemezi. Sitaki wabweteke kwa sababu kaka yao ni mbunge na waziri, wakimaliza kusoma wanakuja kunisaidia kupika na kuuza, kila mmoja anajua biashara hii.”

Ni msaada kwa majirani

Kwa majirani, mama huyo ni kipenzi chao. “Amekuwa msaada mkubwa sana hapa Bweni tangu zamani, anapenda kuwasaidia anaowajua na asiowajua, na niseme tu kwamba upendo wake kwa watu ndiyo uliosababisha mwanaye Jumaa achaguliwe kwa sababu tuliamua kumpa ubunge mtoto wa mamalishe,” anasema Mwajuma Hassan.

Fatma Mtungakoa anasema mbali na kupenda kujichanganya na wenzake bila kuwabagua, lakini pia mama huyo ana sifa moja akitabiri jambo ndilo linalotokea na kwamba anaheshimika eneo hilo kutokana na ukweli kwamba anatoka katika ukoo wa Kisharifu.

“Huyu mama akikuambia ameota kwamba kuna jambo fulani litakutokea, basi ujue litakutokea kweli anaheshimika hapa Bweni kwa hilo,” anasema. “Hana maringo, hivi mama wengine tunaowajua akiwa na mtoto naibu waziri si angetukalia vichwani sisi, lakini huyu hata huwezi kumtambua.”

Waziri Aweso

Katika mikutano mbalimbali ya hadhara ambayo amekuwa akihutubia, Naibu Waziri Awesso amekuwa akieleza kuwa ni mtoto wa mamalishe.

Pia, mara nyingi anapomzungumzia mama yake huwa anapiga magoti kuwashukuru watu waliomwamini na kumchagua.

Akizungumza na Mwananchi jana, Awesso alisema anajivunia kuzaliwa na mamalishe kwa sababu mbali ya kumfundisha kujitegemea katika maisha, lakini kupitia biashara yake ndiko alikolelewa, kusomeshwa na alikopatia fedha za kuchukulia fomu zilizomwezesha kugombea ubunge na kufikia nafasi aliyonayo.

“Najivunia kuwa mtoto wa mamalishe, ananipenda na mimi nampenda, ni msaada mkubwa kwangu, yeye ni kiungo kikubwa baina yangu na wapigakura,” alisema Awesso.

“Kila nikimuuliza mama nikufanyie nini ananiambia furaha yake yeye ni kuona nawatumikia wananchi, sina cha kumlipa, bali Mungu ndiye atakayemlipa.”



Chanzo: mwananchi.co.tz