Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama mdogo asimulia maisha ya Mkapa utotoni

56283a3d5e9502482914e0940fac0227 Mama mdogo asimulia maisha ya Mkapa utotoni

Wed, 29 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMA mdogo wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Rose Magnus Mkapa (94), amesema wakati wa utoto Mkapa alikuwa jasiri, alicheza kwa muda mfupi na alitumia muda mwingi kusoma vitabu baada kutoka shuleni.

Amesema kijini Lupaso kuwa baada ya kutoka shuleni wakati alipokwenda kucheza, Mkapa alipenda kucheza mpira wa miguu tu na si michezo mingine.

Kauli hiyo pia inathibitisha namna Mkapa alivyokuwa shabiki wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam. Rose alisema Kijiji cha Lupaso kilianzishwa na ukoo wa Mkapa pekee wakiishi ndugu wa familia moja kwa malezi ya pamoja, lakini baada ya uhamisho wa vijiji vya ujamaa, walihamia watu kutoka maeneo mengine na kutengeneza jamaa moja wanayoishi kijijini humo mpaka sasa.

Akizungumza na gazeti hili jana nyumbani kwake, Rose aliyezaliwa mwaka 1926, alisema kuwa malezi ya watoto wa kijiji hicho awali yalikuwa ya pamoja, hivyo anamkumbuka vizuri Mkapa alivyokuwa mtoto kuwa alipenda zaidi kusoma kuliko kitu chochote kile.

Alisema kuwa baada ya kutoka shule, Mkapa alitumia muda mwingi kukaa ndani kusoma. Mkapa alisoma Shule ya Msingi Lupaso ya kijijini hapo.

Alisema kuwa kama Benjamin Mkapa angetaka kucheza, alipenda kucheza na baba yake ambaye alidai alimpenda sana na ikiwa angecheza na watoto wenzake kwa muda mfupi, angecheza mpira wa miguu aliokuwa akiupenda sana.

“Katika kijiji hicho awali wote tulikuwa wana ndugu tu, vijiji vya ujamaa viliwaleta watu kutoka mbali hapa na kuwa jamaa moja. Familia yangu na ya dada yangu (mama wa Mkapa) tulikaa wote pamoja, tulijenga sisi hapa wao pale (akionesha nyumba ya Mkapa),” alisema Rose na kubainisha kuwa Mkapa alikuwa jasiri sana.

“Alikuwa jasiri sana sana, hakupenda kujichanganya sana na wenzake maana muda mwingi aliutumia kusoma, alipenda kusoma sana sana.

Marehemu dada (mama wa Mkapa) alikuwa mkali sana kuliko baba yao, hivyo hakuwalea akina Mkapa hovyo hovyo, aliwalea kwa maadili ya dini sana na kusoma sana”alisema.

Alisema kuwa dada yake aliamini kuwa watoto hawana uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe wakiwa wadogo, hakupenda watoto akiwemo Mkapa wachelewe shule na waliporudi alitaka wasome vitabu na kufanya kazi za shule.

Akizungumzia ukaribu wa Mkapa na baba yake kama ulisababisha achague kuzikwa pembeni mwa kaburi la baba yake, Rose alisema alikuwa kipenzi cha baba yake, alipenda kucheza naye na alitumia muda mwingi kuwafundisha Mkapa na ndugu zake mafundisho ya dini.

Kauli ya Rose inathibitishwa na kazi ya baba yao, mzee William Matwani kuwa alikuwa Katekista (mwalimu wa dini) katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kijijini hapo.

Alisema kuwa ana uchungu mkubwa kwa kifo hicho na mara kadhaa katika mahojiano, alionekana mwenye uchungu mwingi alipozungumza kitandani alipokuwa amekaa, nyumbani kwake ambako kutoka nyumba alikozaliwa Mkapa ni urefu wa kama mita 100 hivi.

Rose alisema ikiwa watu wanamfahamu Mkapa kama mtu mkali kwa mambo ya rushwa na yasiyo ya maadili, basi ukali huo amerithi kwa mama yake, Stephania Nambanga aliyefariki dunia Juni 29 mwaka 1991.

Katika eneo la sala, mama mdogo Rose alithibitisha kuwa familia ya Mkapa ni ya kiimani ambapo baada ya mahojiano na waandishi kumalizika, aliwaongoza waandishi kusali sala fupi iliyohusisha Sala ya Baba Yetu mara tatu, Salamu Maria mara mbili na kumalizia na Sala ya kuomba Mkapa apokelewe mahali pema isemayo Raha ya milele umpe eee bwana na mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani, amina.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema kuwa Mzee Mkapa alikuwa mtu anayependa kusoma na alipenda hata watu wa chini yake wasome.

“Mkapa nimefahamiana naye siku nyingi sana, alikuwa rafiki yangu na alinisaidia mambo mengi. Mimi wakati nikiwa DC (Mkuu wa Wilaya ya Masasi) yeye alikuwa Mbunge wa Nanyumbu na alinipokea nilipoteuliwa kuwa DC Ilala na baadaye alipokuwa madarakani aliniteua kuwa Mkuu wa Mkoa Tanga kwa miaka mitano.

“Kwa muda wote niliomfahamu nilipofanya naye kazi, alikuwa akikupa kazi, anakupa uhuru akiamini kuwa utaifanya ipasavyo.

Lakini Mkapa alipenda sana kusoma vitabu, wakati wa uongozi wake sisi tuliokuwa Ma-RC alituletea mpaka makala ili tusome na kujua mambo mbalimbali ya kiuchumi yanayoendelea,” alisema Mkuchika.

Chanzo: habarileo.co.tz