Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama huyu apata masahibu makubwa, aomba msaada

60273 Pic+mama

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Siku zote asemaye yanayomsibu hupata ufumbuzi kwa haraka, hivyo ndivyo ilivyo kwa Neema Isaya (21), mkazi wa kitongoji cha Mapinduzi wilayani Serengeti mkoa wa Mara ambaye titi lake linatoka nyama.

Neema mwenye watoto wawili wa kike, mmoja akiwa wa miezi mitatu, anaomba msaada wa matibabu kutokana na tatizo hilo la titi ambalo madaktari wa Hospitali Teule ya Nyerere wameshindwa kujua ugonjwa unaomtafuna na kutakiwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uchunguzi zaidi.

Akizungumza na Mwananchi jana huku akilia kwa maumivu, Neema alisema anahofia maisha yake kutokana na tatizo hilo.

Akiwa katika hali ya kukata tamaa baada ya madaktari kushindwa kubaini ugonjwa unamsibu huku mwenyewe akihisi ni saratani, alisema hana uhakika kama atakwenda Bugando kwa kuwa hana fedha.

“Nimeambiwa nikachunguzwe Bugando Mwanza kama ni saratani, sijui kama watanikata titi. Naomba sana watu wanisaidie ili nikapate matibabu mapema kwa kuwa kila siku nyama zinazidi kutoka. Sijui ni kiasi gani kinahitajika kwa ajili ya matibabu na chakula maana sina ndugu Mwanza,” alisema.

Neema alisema tatizo hilo lilianza mara baada ya mtoto wake kumcheulia wakati ananyonyesha na titi kuanza kuvimba.

Pia Soma

“Mama yangu na majirani waliniambia hilo ni jambo la kawaida litapona nikaendelea na matibabu ya kawaida ikiwamo kukanda kwa maji ya moto, lakini hali ikawa inazidi kuwa mbaya,” alisema.

Alisema baadaye ilionekana kuwa ana jipu na kuamua kwenda Hospitali Teule ya Nyerere likapasuliwa na kupewa dawa na kuingiziwa gozi.

Alisema hospitali walimwambia awe anakanda kwa maji ya chumvi ya uvuguvugu lakini tangu wakati huo kila kukicha akawa anaona nyama zinazidi kudondoka.

“Kutokana na maumivu ninayoyapata usiku nashindwa kulala, natamani kwenda haraka Bugando lakini sina bima ya matibabu ambayo ingenisaidia na mama yangu ni mlemavu wa miguu,” alisema.

Kaimu Mganga Mkuu Wilaya ya Serengeti, Emiliana Donald alisema kwa kuwa Neema hana bima ya afya anatakiwa awe na fedha kwa ajili ya nauli na kujikimu kwa muda ataokuwa Bugando.

Neema ameomba kwa watakaoguswa na tatizo lake wawasiliane na mwandishi kwa habari hii kwa namba ya simu 0713-961399 au 0759-891849.

Chanzo: mwananchi.co.tz