Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama auza nyumba kumtibu mwanaye aliyevunjika mgongo

49950 NYUMBA+PIC

Tue, 2 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Uchungu wa mama kwa mwanaye ndio uliomsukuma Ndesi Kyeja, mkazi wa Kijiji cha Ngeleka, Busokelo wilayani Rungwe kuuza nyumba na mali zake ili kunusuru uhai wa mwanaye Lusubilo Sinunu (18) aliyevunjika uti wa mgongo.

Lusubilo alivunjika mgongo Januari 3 baada ya kudondoka kutoka mti ulio jirani na nyumbani yao wakati akipunguza matawi ya mti huo. Hata hivyo, nyuma ya mkasa huo Ndesi alilazimika kuuza mali zake ili kunusuru uhai wa mwanaye.

Mwananchi lilifika Hospitali ya Rufaa Mbeya kuzungumza na mama huyo pamoja na mwanaye aliyekuwa amelalia tumbo muda wote.

Lusumbilo anasema siku ya tukio saa sita mchana akiwa nyumbani kwao aliombwa na jirani yao amsaidie kukata matawi juu ya mti.

Anasema baada ya kupanda juu alikata tawi moja na alipojaribu kukata la pili aliteleza na kudondoka chini.

“Baada ya kupanda juu yule jirani alinipa kamba nikishakata tawi nilifunge ili lisidondokee choo. Nilikata tawi la kwanza na nilipotaka kukata la pili niliteleza nikaanguka na kufikia mgongo,” anasema Lusubisyo.

Baada ya kuanguka, mama wa jirani aliyemtuma kukata matawi alimpeleka zahanati ya kijiji wakati akiwa hana fahamu.

Wakati Lusubilo akipatwa na tatizo hilo, mama yake alikuwa shambani na aliporudi alipewa taarifa.

Maelezo ya mama, daktari

Baada ya kurejea nyumbani, Ndesi, mama wa Lusubilo anasema, “niliacha kila kitu nikakimbia kumfuta huko (zahanati).”

Anasema baada ya kufika alimkuta akiwa na hali mbaya na baada ya kuzinduka alianza kulalamika maumivu makali ya mgongo.

Anasema jirani aliyekuwa akisaidiwa na Lusubilo alichangia Sh10,000 kulipia huduma ya kwanza kabla ya kuambiwa waende Hospitali ya Matema wilayani Kyela. “Mtoto wangu alilala zahanati na siku iliyofuata akaja daktari aliyehoji kwa nini tunamchelewesha kumpeleka Matema wakati kaumia sana na tatizo lake si la kutibiwa hapo. Na hapo nikahangaika kukodi gari hadi Matema.”

Anasema baada ya kufika huko madaktari walimweleza tatizo ni kubwa hivyo waende Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

“Basi hapo wakasema nikodi gari lao (hospitali), kwa kweli nikashindwa gharama zao nikalazimika kukodi gari ya kawaida hadi hapa Mbeya, na nilipofika hospitalini nikapokewa na madaktari wakampiga x-ray mara mbili, lakini majibu hayakupatika na mara ya tatu ndipo ikatoa majibu kwamba amevunjika uti wa mgongo,” anasema.

Anasema baada ya majibu madaktari walishauri ampeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa vile tatizo lake ni kubwa, lakini kutokana na kutokuwa na uwezo kifedha alishauriwa arudi nyumbani na mtoto hadi atakapopata fedha. “Nikakodi gari kurudi nyumbani ili nikajipange tu, lakini nikiwa njiani mtoto alianza kubadilika hali ikawa mbaya zaidi, hapo dereva akanishauri nisiende naye na kwa hali ilivyo tunyooshe moja kwa moja Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana.”

Anasema akiwa nje ya hospitali hiyo daktari mmoja alimshauri aende ofisi za ustawi wa jamii ambako alisaidiwa kurejeshwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Huko mwanaye alitibiwa vidonda na pia walimgharamia fedha za chakula na malazi katika nyumba ya kulala wageni.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Lazaro Mboma anasema Lusubilo alivunjika uti wa mgongo na kumfanya ashindwe kutembea. “Lakini mbali na hilo alipata kidonda na baada ya kurudi tena hapa kwetu tuliendelea kumtibu na hadi sasa hali yake inaendelea vizuri, lakini tunaona ni vyema aende Muhimbili kitengo cha mifupa na tunataraji kuwa atawekewa vifaa vitakavyomwezesha kukaa.

Auza nyumba na mali zake

Ndesi anasema ili kuhakikisha mtoto wake anapata matibabu alilazimika kuuza nyumba kwa Sh300,000 pamoja na pia kuuza kuku, ng’ombe, nguruwe na vyombo vya ndani. “Tangu siku ya tarehe 3 mwezi wa kwanza nilipoondoka sijawahi kurudi (nyumbani) hadi leo, hivyo vitu vyote nilivyouza nilikuwa ninawaagiza watoto wangu wauze na wanatumia fedha, niliuza nyumba yangu Sh300,000, ng’ombe wawili Sh350,000, nguruwe wawili Sh140,000, kuku watano Sh40,000 lakini nikauza vitu vyote vya ndani kwa Sh200,000,” anasema.

Baada ya kuuza nyumba yake, anasema yule mteja aliyeinunua aliwaonea huruma watoto wake hivyo aliwaacha waendelee kuishi.

Katibu wa watalamu wa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Gerald Mwaulesi anasema walichangishana fedha na kuikomboa nyumba hiyo pamoja na kumlipia Ndesi madeni aliyokuwa anadaiwa.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ambaye alifika Hospitali ya Rufaa Mbeya kumjulia hali kijana huyo aliamua kuchukua jukumu la kumsafirisha hadi Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Jana, Dk Tulia aliliambia Mwananchi kuwa Lusubilo alipokewa hospitalini hapo na kufanyiwa upasuaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz