Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama asimulia mwanaye alivyonusurika kifo baada ya kukatwa koromeo

40719 Pic+koromeo Mama asimulia mwanaye alivyonusurika kifo baada ya kukatwa koromeo

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Njombe. Mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema, Njombe Mji, Rabia Mlelwa amesema mtoto wake Meshack Myonga (4) alinusurika kimiujiza kuuawa baada ya kutekwa na mtu asiyejulikana.

Alisema tukio la kutekwa kwa mwanaye huyo lilitokea saa tano asubuhi, Desemba 23, mwaka jana, na alikatwa koo kisha kutelekezwa kwenye moja ya misitu ya miti iliyopo katika kata hiyo kabla ya kuokotwa na kijana mmoja.

Ilivyokuwa

Rabia alisema siku hiyo alitoka kumuandikisha mtoto huyo shule ya awali na alipofika maeneo ya nyumbani, alipita nyumba ya jirani kumjulia hali mama aliyekuwa ametoka kujifungua, lakini Meshack alimuambia kwamba anakwenda nyumbani kwa vile baba yake alikuwapo.

“Ni kama hatua 30 tu na nyumbani kwetu, nikasema haya tangulia,” alisema.

Alisema alipofika nyumbani hakumkuta ndipo alipomuuliza mumewe Meshack alipokuwa akaambiwa tangu walipoondoka wote hajarudi.

“Nilijua pengine amepitia kwa watoto wenzake kucheza, nilikaa lakini nikaona roho inaniuma mwanangu yuko wapi, nikaanza kumuulizia kwa majirani, ilipofika saa 12 jioni, nikaenda kwa balozi”.

Alisema walipoendelea kumtafuta, mtu mmoja akumueleza kwamba kuna mtoto ameokotwa huku akiwa amechinjwa shingoni, pengine ndiye huyo maana wazazi wake hawajafahamika.

“Yule mama (aliyetoa taarifa za kuonekana kwa mtoto) akaniuliza kwani mtoto wako alivaaje? Nikamuelezea alivyokuwa amevaa, akasema basi ndiyo huyo ameokotwa msituni na amepelekwa Hospitali ya Kibena. Tukaenda hospitali hapo tukaambiwa ameandikiwa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.”

Rabia alisema asubuhi na mapema ya siku iliyofuata, yeye na mumewe walikwenda kituo cha polisi kutoa maelezo na baada ya hapo wakamfuata mtoto Mbeya ambako walimkuta akiwa na mama mmoja msamaria ambaye alitoa msaada tangu alipomkuta Meshack katika eneo la tukio ambako alimfunga kanga na kumpeleka hospitali ya Kibena.

“Nilimkuta mwanangu akiwa chumba cha mahututi huku akiwa haongei, hivyo nikampokea yule mama akarudi Njombe na mimi nikabadi na mtoto hospitalini hapo na tulikaa wiki mbili,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Mtaa wa Mji Mwema, Alanus Mwalongo alisema baada ya kuokotwa, wasamaria walikwenda naye hospitali, “baada ya michakato yote, nilitoa taarifa polisi tukatakiwa twende polisi na wazazi wa mtoto kwa ajili ya kuandika maelezo.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa matukio yote ya kutekwa na kuuawa watoto wilayani Njombe na watu 28 wanashikiliwa.

Hali yake

Rabia alisema hivi sasa mtoto wake anaendelea vizuri tofauti na awali ambako alikuwa anashindwa kuhema kutokana na koo lake kuharibiwa kwa kuchinjwa.

“Unamuona anavyohema kama mtu mwenye mafua (huku akimwangilia Meshack), lakini bora sasa hivi, huko nyuma alikuwa anahema kwa taabu mno. Sasa tunaendelea na matibabu nyumbani kwa kufuata maelekezo ya daktari na kesho (leo) tunarudi tena Mbeya (hospitali) kwa ajili ya uchunguzi,” alisema Rabia.



Chanzo: mwananchi.co.tz