Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama asimulia alivyopata taarifa kifo cha mwanaye aliyefia baharini

9428 Pic+mama TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mama wa Queen Madala (17), aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita alipokuwa akiogelea na wenzake eneo la Kimbiji wilayani Kigamboni, amesema ndoto za mwanaye kuwa polisi zimezimika kama mshumaa uliopulizwa na upepo.

Happy Mathew (38), ambaye ni mfanyabiashara ndogo alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni siku moja baada ya kumzika mwanaye eneo la Kongowe wilayani Temeke.

Queen na wanafunzi wenzake watatu wasichana wa Sekondari ya Kimbiji walifariki dunia Jumamosi wakiogelea ufukweni mwa Bahari ya Hindi eneo la Kimbiji.

Walipelekwa eneo hilo na walimu wao kuwapongeza wenzao waliofanya vizuri katika mtihani wa majaribio (mock).

Mzazi huyo alisema licha ya tukio hilo kutokea siku hiyo, hakupewa taarifa na uongozi wa shule badala yake alielezwa na wanafunzi. “Ijumaa (Queen) alinipigia simu na kunitaarifu kuwa walimu wameamua kuwapeleka wakafurahi baada ya kufanya vizuri katika mitihani yao, sikuwa na kipingamizi kwa sababu niliamini kuna ulinzi wa kutosha,” alisema Happy. Alisema mwanaye aliyekuwa mtoto wa pili kati ya watatu alikuwa na tabia ya kumpigia simu kumjulisha alichokuwa akifanya, lakini haikuwa hivyo siku ya tukio.

“Nilishangaa jioni imefika lakini hakuniambia ilikuwaje, jambo ambalo lilinitia wasiwasi na hasa aliponipigia simu rafiki yake na kuniuliza kama Queen ni mzima,” alisema.

“Nilishtuka na kumuuliza nini kimetokea ndipo akaniambia. Nilijaribu kutafuta ukweli lakini walimu sikuwapata badala yake nilipigiwa simu na ofisa upelelezi kutoka kituo cha polisi Temeke aliyenipa taarifa hizo.”

Alisema Queen alikuwa akifanya vizuri darasani jambo lililomfanya aongeze bidii katika biashara ili aweze kumlipia ada.

“Nimekuwa nikihangaika leo maandazi, kesho vitumbua ili mwanangu asome lakini imeshindikana,” alisema

Chanzo: mwananchi.co.tz