Severa Tesha (32) mkazi wa Kijiji cha Ubetu, Kata ya Ubetu Kahe, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro amemchoma mwanaye kwa panga lenye moto sehemu za mapajani na kumsababishia majeraha na maumivu makali.
Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ubetu amefanyiwa ukatili huo na mama yake mzazi kwa madai ya kutoosha vyombo ambavyo aliagizwa avioshe.
Mpaka sasa mwanafunzi huyo ameshindwa kwenda shule kutokana na majeraha. Akizungumzia tukio hilo Mei 11,2022 Mwalimu wa malezi wa shule hiyo, Notibruda Massawe amesema baada ya kufanyika tukio hilo mama mzazi wa mwanafunzi huyo alipiga simu shuleni akidai mwanaye huyo anajipu hawezi kutembea.
"Huyu mama alitoa taarifa shuleni kwamba mwanaye ana jipu hawezi kutembea kufika shuleni,lakini baadaye ndugu zake walipiga simu kwamba huyu mtoto amechomwa na mama yake mzazi," amesema.
"Na sisi kwa kujiridhisha tulienda kumuona na tumekuta amejeruhiwa mapaja yote mawili na hawezi kutembea lakini kwa sasa anaendelea na matibabu," amesema.
Naye msaidizi wa masuala ya Kisheria Wilaya ya Rombo, Remmy Shirima amesema baada ya kupata taarifa hizo alifika nyumbani kwa mama huyo ambapo baada ya kuona mtoto huyo amejeruhiwa alitoa taarifa polisi na mama huyo alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Usseri.
Mpaka sasa mama huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na tukio hilo.