Tabora. Mwanamke anayedaiwa kuua watoto sita na yeye kufariki katika mazingira ya kutatanisha, aliomba mganga wa kienyeji amruhusu kwenda kuwasalimu watoto hao kabla ya kufanya tukio hilo, imeelezwa.
Mama huyo, Nana Maganga, 35, aliua watoto wake watano na mmoja wa kaka yake kwa kuwakata kwa panga mwishoni mwa wiki iliyopita, kabla ya yeye kufariki dunia. Hata hivyo kifo cha mama huyo bado kina utata kutokana na maelezo ya watu waliomdhibiti kuwa walimkamata na kumfunga kamba, lakini baadaye alikunywa sumu, jambo ambalo Jeshi la Polisi halijakubaliana nalo na linawashikilia watu watano kwa mahojiano.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi alfajiri katika kitongoji cha Mwakilezu, kijiji cha Luzuko, kata ya Mizibaziba wilayani Nzega.
Diwani wa Mizibaziba, Modesta Robert aliiambia Mwananchi kuwa Nana alikuwa ni mchapakazi, lakini alianza kupata matatizo ya akili takriban mwaka mmoja uliopita.
Baada ya kuugua, baba yake, ambaye hakumkumbuka jina alimchukua na kumpeleka eneo linaloitwa Mila ambako kuna mganga wa kienyeji.
Baadaye, kwa mujibu wa diwani huyo, Dotto Jisenge, ambaye ni mume wa Nana, alishindwa kuishi na watoto wao waliokuwa saba baada ya mkewe kuondoka, na ndipo akaamua kuwapeleka kwa kaka yake aitwaye Mashaka Jisenge.
Alisema wakati akitibiwa kwa mganga huyo wa kienyeji, Nana aliwaeleza kuwa anataka kwenda kuwaona watoto wake waliopelekwa kwa shemeji yake, yaani Mashaka aliyekuwa akiishi umbali wa kilomita tano kutoka kwa mganga.
Alisema aliruhusiwa na kwenda kwa shemeji yake ambako alifika usiku na kuandaliwa sehemu ya kulala pamoja na watoto hao.
Kukiwa kunakaribia kupambazuka, majira ya saa 11:00 alfajiri, Mashaka na mkewe walisikia kelele kutoka kwa watoto waliokuwa wakisema “mama unatuua” na walipokwenda walikuta hali ikiwa mbaya.
“Mashaka na mkewe walipokwenda walimkuta Nana mlangoni akiwa na panga huku mtoto wa Mashaka aitwaye Pala Masanja (3) akikimbia,” alisema.
“Alikatwa na panga kiunoni hadi uti wa mgongo na kufariki. Ilibakia kidogo atenganishe kiwiliwili.
“Tukio hilo ndilo lililofanya watafute watu wengine na kumdhibiti ingawa mimi tayari nilikuta Nana ameshafariki wakati nilipofika.”
Diwani huyo alisema wote waliofariki walizikwa Jumamosi jioni na waliojeruhiwa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Nzega. Diwani huyo alisema hali zao zinaendelea vizuri.
Tukio hilo halikutegemewa, lakini maisha ya Nana yalishangaza wengi kutokana na jinsi alivyokuwa akifanya kazi ambazo si wengi wanaozimudu.
Akizungumzia maisha yake, Diwani Modesta alisema Nana alikuwa akifanya biashara ya mkaa, lakini tofauti na wanawake wengine wanaofanya kazi hiyo, alikuwa akienda kuuchoma mwenyewe.
“Alikuwa akikata magogo na miti mikubwa kwa ajili ya kuchoma mkaa,” alisema diwani huyo.
“Pia alikuwa akilima eneo kubwa bila kuchoka. Kwa kweli alikuwa na nguvu zisizo za kawaida hata kuwazidi wanaume wengi na kufanya kazi pasipo kuchoka.”
Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa wilaya, Godfrey Ngupulla alisema Nana alikuwa akienda kwa shemeji yake mara kwa mara na kwamba siku hiyo, lakini siku ya tukio hilo alikuwa na pilikapilika zisizokuwa za kawaida.
Alisema inaelekea siku hiyo kulikuwa na wanawake peke yao na hivyo kupata msaada ilikuwa kazi ngumu kwa vile nyumba zipo umbali mrefu sio kama maeneo ya mjini.
Kauli hiyo inalingana na ya mtendaji wa kijiji cha Luzuko, Neema Gidarya aliyesema kufika eneo la tukio ni mbali na njia yake ni mbaya.
Lakini alisema Nana alikuwa na mapepo na sio kichaa wa kuokota makopo.
Girdaya pia alisema Nana alitoroka kwa mganga ili akasalimie watoto wake.
Kuhusu watu watano walio mahabusu wakihojiwa kuhusu mauaji hayo, kamanda wa polisi wa Tabora, Emmanuel Nley alisema wanaendelea kuwashikilia kwa mahojiano Masanja Jisenge na kaka yake Dotto Jisenge ambaye ni mume wa marehemu na wanandugu watatu, Mapande Kulingwa, Mafuta Tungu na Paul Penda.
Soma zaidi: Mama aua watoto sita, mwenyewe afariki