Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama akatwa mkono, mtoto ajeruhiwa kichwani

Mkono Pic Mama akatwa mkono, mtoto ajeruhiwa kichwani

Thu, 10 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi Kata ya Mkindi, wilayani Kilindi; mkoani Tanga, Tabu Mokiwa, amekatwa mkono huku mtoto wake akijeruhiwa kichwani, baada ya kudaiwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Akizungumzia tukio hilo, mtoto Halima Shabani, amesema walivamiwa na watu usiku, ambao wanadhani ni wafugaji ambao inadaiwa walimshambulia mama yake hadi kumkata mkono, na kwamba alipojaribu kumsaidia, naye alikatwa mara tatu kichwani.

Amesema watu hao walianza kwa kupiga hodi na mama yake kuuliza ni wakina nani, ila watuhumiwa hao walilazimisha mlango ufunguliwe, na kwamba familia hiyo ilipogoma, ndipo watuhumiwa wanadaiwa kuvunja mlango huo.

Mtoto huyo ameongeza kuwa baada ya kuvunja mlango walimuuliza mama yake kuwa kama yeye ndiye Tabu na alipojibu kuwa niyo yeye, inasemekana watu hao walianza kumshambulia mama huyo kwa kumkata na vitu vinavyosadikiwa kuwa nan cha kali.

"Mama wamemkata mkono kabisa nilipoona wanazidisha nilimsaidia, lakini na mimi nilikatwa kichwani na mkononi, wote tumeumia sana, ila mama kapoteza mkono wake,” amesema Halima.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa analifuatilia kupata taarifa zaidi kwani yupo safarini na kwamba atatoa taarifa kamili kuhusu tukio hilo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Handeni, Hudi Shehdadi, amekiri kupokea majeruhi wawili wa tukio hilo na kwamba wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.

Naye mkazi wa Kata ya Mkindi, Rajabu Lukuwa, amesema kwa sasa hawana amani na kwamba wanaishi kwa hofu kutokana na matukio kama hayo.

Kwa maelezo ya majeruhi hao, chanzo cha ugomvi huo ni mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kata ya Mkindi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live