Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama ajifungua pacha watatu Geita, afikisha wanane

Pacha2pic Mama ajifungua pacha watatu Geita, afikisha wanane

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Ikurwa Wilaya ya Geita, Rebeka John (27) amejifungua watoto watatu waliozaliwa kabla ya muda (njiti) katika Kituo cha Afya Nyankumbu kilichopo Mjini Geita.

Rebeka aliyejifungua Machi 4, 2024, ameomba wasamaria wema kumsaidia ili aweze kupata mahitaji ya watoto wake, hususan maziwa.

Mama huyo ambaye pacha wake wapo chini ya uangalizi maalumu kutokana na wao kuzaliwa na uzito pungufu, amesema changamoto kubwa aliyonayo kwa sasa ni ukosefu wa maziwa na nguo.

Akizungumza nasi, jana Alhamisi, Machi 7, 2024 hospitalini hapo, Rebeka ambaye awali alikuwa na watoto wengine watano, amesema hakutarajia kujifungua mapacha na kuwa alianza kliniki ujauzito wake ukiwa na miezi sita katika Zahanati ya Ikurwa, iliyopo mjini Geita na wakati wa mahudhurio watoa huduma walimtaka akajifungulie Kituo cha Afya Nyankumbu, lakini hawakumweleza sababu.

“Changamoto niliyonayo ni upungufu wa maziwa, mume wangu ni mkulima hana uwezo wa kununua maziwa ya kopo, naomba wasamaria wanisaidie, maana hata sasa maziwa ninayotakiwa kukamua hayatoshi kipimo nilichoambiwa,” amesema.

“Kuwalea naweza ila matumizi ndio shida, mume wangu ni mkulima amemshukuru Mungu kuwapata, lakini ndio tunajiuliza hawa watoto tutawapa nini maisha yetu ni ya chini sana,” ameongeza.

Mama huyo amesema mtoto wake wa kwanza ana umri wa miaka 12, mwingine miaka 10, anayefuata miaka nane. Mtoto wa nne ana umri wa miaka sita na mdogo miaka mitatu na wote wanahitaji uangalizi.

Kwa upande wake, Kurwa Ludewa, mama mkwe wa Rebeka ameomba Watanzania wamsaidie ili waweze kuwalea watoto hao kwa kuwa wanaishi maisha duni na hata hao waliozaliwa hawana nguo na maziwa hayatoshi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyankumbu, Irene Temba amesema walimpokea mama huyo Machi 2, 2024 akiwa na mimba ya wiki 31 akiwa na uchungu na walimwanzishia matibabu ya kukomaza mapafu ya mtoto na dawa ya kuzuia uchungu.

Amesema akiwa wodini, Machi 4 saa nne usiku alipata uchungu na kujifungua watoto watatu, mmoja akiwa na kilo 1 na gramu 600 wa pili alizaliwa na kilo moja na watatu akiwa na gramu 900.

Dk Temba amesema changamoto inayoendelea sasa ni mama kuwa na maziwa kidogo yasiyowatosheleza watoto hao.

“Mama anaendelea vizuri lakini uzito tunaotegemea wawe wamefikia bado umepungua na jinsi maziwa yake yanavyotoka itakuwa changamoto, maana maziwa anayokamua hayafiki mahitaji ya hawa watoto.

“Tunawakadiria kutokana na kilo zao, mama anakamua tunawanywesha lakini kipimo tunachotaka hakitoshelezi,” amesema Dk Temba.

Kwa mujibu wa Dk Temba, mara nyingi kituoni hapo huzaliwa watoto pacha, lakini kwa mama kujifungua watoto watatu, kwake ni tukio la kwanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live