Lindi. Mbunge wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa bati, chakula, mavazi, sabuni pamoja na maturubai kwa wahanga wa mafuriko mkoani Lindi.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mama Salma leo Jumapili Februari 2, 2020, Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi, Rukia Hassani kwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Mama Salma, ameguswa na tatizo lililotokea hivyo ametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa waathirika hao.
Rukia amesema Mama Salma amejitolea kutoa msaada huo kwa jamii iliyokumbwa na maafa hayo baada ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya Lindi vijijini, Kitomanga na Nangaru.
Amesema juhudi za makusudi zinahitajika kuchukuliwa kutokana na waathirika hao kuhitaji misaada ya kijamii kama ya makazi chakula , mifugo na mazao yao kusombwa na maji.
“Hatuna budi kutoa shukrani kwa msaada wake kwani hii inaonyesha anajali wananchi kwa moyo wa uzalendo,” amesema Rukia.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Ndemanga amesema Mama Salma ameonyesha moyo wa kuwathamini jamii yenye matatizo na kujali janga la mafuriko ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kimaendeleo na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano huo.
Pia Soma
- Mfanyabiashara akutwa amejinyonga Arusha
- Lema amtaka Waziri Simbachawene ajiuzulu
- ACT – Wazalendo: Wabunge wa CCM watawajibika lolote likimtokea Zitto
Ndemanga amesema pamoja na misaada inayotolewa serikali imetenga maeneo ya viwanja ambavyo vitagawiwa kwa wananchi wote waliokumbwa na mafuriko ili wakaendelee na shughuli zao za kuwaletea maendeleo.