Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama Lishe alivyoienzi Siku ya Wanawake

45717 Pic+wanawake Mama Lishe alivyoienzi Siku ya Wanawake

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dra es Salaam. Bahati Rajab anakatakata bamia, pembeni ya jiko la mkaa lililo na sufuria iliyo na kitoweo anachoandaa kwa ajili ya wateja wake.

Hana sehemu nzuri ya kufanyia biashara hiyo. Amejipachika pembeni ya kituo cha daladala cha Tabata Relini, akitegea waendesha bodaboda wanaotoa huduma kwa abiria wanaoshuka kutoka kwenye mabasi kwenda sehemu za ndani za Tabata Kisiwani na kwingineko.

Anajua kuwa jana ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake na anajua changamoto ambazo wanawake wanakabiliana nazo, lakini hajui ni jinsi gani ataienzi, badala yake anaamua kuendelea na shughuli zinazomuwezesha kupeleka mkono kinywani.

“Naifahamua kuwa hii ni siku yetu wanawake ambayo inatakiwa kutukomboa kimaisha, kimabadiliko na kimaadili na kujua mwanamke afanyaje ili kujikwamua kiuchumi,” anasema Bahati, mwanamke wa makamo na mchangamfu.

“Wanawake tuna changamoto nyingi katika biashara tunazofanya, kama mimi ambaye ni mama ntilie (muuza chakula). Utakuta watu wanajua nauza chakula bei gani kwa sahani, lakini anatokea mtu hasa wanaume anakupa hela pungufu tena makusudi. Sasa hapo mpaka muanze kugombana ndio atoe hela kamili, jambo ambalo si zuri.”

Bahati anapika ugali, wali, nyama, maharage na mbogamboga kulingana na chaguo la mteja na anauza Sh1,500 kwa sahani moja.

“Kwa siku naweza kupata kati ya Sh40,000 na Sh50,000. Angalau zinaniwezesha kuishi,” anasema.

Lakini, kama mfanyabiashara, anaona baadhi ya kero zimepungua baada ya kupata Kitambulisho cha Mmachinga.

“Namshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogondogo,” anasema.

“Vimetusaidia sana kufanya biashara kwa uhuru tofauti na zamani tulipokuwa tunanyanyasika sana. Ukifanya biashara sehemu kama hii barabarani unafukuzwa. Lakini tunachomuomba atusaidie wanawake kupata mikopo ili kukuza biashara zetu.”

Bahati amewataka wanawake kuzidi kujituma kwa kuwa ndio tegemeo kubwa kwa familia zao.

Mwanamke mwingine, Maua Ulaiti ambaye anauza vinywaji laini, anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni wanaume kuwadharau na kuwaona wana kipato kidogo.

“Nishawahi kuhudhuria hata kongamano katika siku kama hii (ya wanawake). Wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi, hasa sisi wafanyabishara ndogondogo. Wanaume wanatudharau na kutuona kuwa hakuna tunachoingiza zaidi ya kupoteza muda tu,” anasema.

“Pia wanaume wengine majumbani wamekuwa wakitufikiria vibaya kwa kuona unapotoka nyumbani na kwenda kufanya biashara, huendi kwa lengo hilo, bali kwa wanaume wengine.”

Bahati na Maua ni kati ya wanawake wengi wa wa kima chake ambao baadhi walijua maadhimisho ya Siku ya Wanawake lakini hawakuona jinsi inavyowagusa na wengine kutojua kabisa.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake huadhimishwa Machi 8 kila mwaka kwa shughuli mbalimbali. Mwaka huu kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa, iliyorasimisha siku hiyo mwaka 1975, ni “Fikiria Usawa, Jenga Umakini na Ubunifu kwa Ajili ya Mabadiliko,” ujumbe ambao unataka kuwepo na usawa wa kijinsia katika kila nyanja.

“Huku teknolojia na ubunifu ukizidi kuwa sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, si rahisi kufikiria maendeleo bila ya vitu hivyo,” linasema tamko la Umoja wa Mataifa.

“Kauli mbiu ya mwaka huu kwa ajili ya Siku ya Wanawake... inalenga kutumia njia ambazo ubinifu unaweza kusaidia kufanikisha usawa wa kijinsia, kuongeza uwekezaji katika maeneo yenye mfumo wa kijamii unaojali usawa wa kijinsia na kuboresha huduma za jamii na miundombinu kwa njia ambayo inakidhi mahitaji ya wasichana na wanawake.”

Kwa Tanzania, kaulimbiu ya mwaka huu ni “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu” na Serikali ilipanga maadhimisho hayo kufanyika katika ngazi ya mkoa ili kutoa wigo mpana kwa wanawake, wadau mbalimbali na kila Mtanzania kutathmini hatua zilizofikiwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz