Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malkia wa nguvu anayeishi kwa kutegemea ‘chupa chakavu’

15143 Pic+malkia TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Glory Silayo, si jina jipya miongoni mwa wengi. Mwanadada huyo, mkazi wa Arusha alianza kusikika zaidi baada ya kuibuka Malkia wa nguvu katika mashindano ya Clouds Media mwaka huu.

Ubunifu wake wa kukusanya taka na kuzipa thamani ndiko kuliko mng’arisha zaidi.

“Jalala lina manufaa sana kwangu, huwa naokota chupa ambazo tayari zimetumika nazipa thamani ili ziweze kutumika tena,” anasema Glory.

Katika simulizi ya maisha yake mbele ya kongamano la ‘Asante Mama’ lililofanyika mkoani Arusha likiandaliwa na Mtandao wa Wasanii wa Muziki wa Injili (Tagoane), Glory alisema ubunifu, kujituma na uwezo wa kutambua na kuchangamkia fursa vimempa faida katika maisha yake.

Anasema mwaka 2015 alipata msukumo wa kuanza kutumia chupa zilizotumika baada ya kupitia changamoto nyingi za kuajiriwa.

“Ilibidi tu nijitose kwenye ujasiriamali, mara ya kwanza nilianza kwa kuuza mkaa,” anasema.

Glory anasema alikuwa akihifadhi mkaa kwenye mifuko mizuri na kuwasambazia wateja, biashara ambayo hakudumu nayo muda mrefu. “Baadaye nilibuni ajira hii ninayoifanya sasa, kukata tamaa siyo maisha na dunia ya sasa inahitaji ubunifu wa juu sana, hivyo nilipoona mkaa unasuasua nikaja na wazo jingine la kubadilisha chupa kuwa mapambo.”

Alianza kwa kujaribu, lakini kadri siku zilivyokuwa zikisogea ubunifu wake ulianza kupata kibali machoni kwa watu wengi.

“Watu walianza kuulizia mapambo nayotengeneza, mtaji wangu ukakua na nikaanza kupata jina kupitia kazi hii ambayo wakati naanza wengine walinishangaa,” anasimulia.

Anasema ukweli ni kwamba chupa za glasi na plastiki zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.

“Kwa hiyo kupitia kazi yangu ya kuzipatia chupa hizi thamani nachangia kwa kiasi kikubwa utunzaji wa mazingira.”

Anasema kuna wakati watu huwa wanamshangaa pale anapoamua kwenda majalalani kuokota chupa hizo, lakini hilo huwa halimtishi.

“Hata kama watu wananiangalia, nikiona chupa huwa sioni haya kuikotoka. Naokota, naisafisha na kuitumia vizuri.”

Faida alizopata

“Nilipata ajira inayonisaidia kukidhi mahitaji yangu ya kila siku, sina wasiwasi tena na kipato,” anasema Glory.

Anasema ametumia fursa hiyo kuwasaidia vijana wengine wanaolia kwa kukosa ajira. “Siyo tu kwamba nawafundisha vijana wenzangu ubunifu, nimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana wenzangu. Namshukuru Mungu kwa sababu badala ya kuajiriwa nimeweza kuwaajiri.”

Anasema zamani haikuwa rahisi kuwasogelea viongozi hasa wakubwa, lakini baada ya kushinda nafasi ya kuwa Malkia wa nguvu amekuwa akipewa nafasi ya kuzungumza mbele yao. “Chupa zangu huwa zinatumika kama zawadi maalumu kwa viongozi, hili linanipa furaha.”

Nini malengo yake

Malkia hiyo wa nguvu anasema yupo kwenye mkakati wa kufungua kiwanda kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata taka zote za glasi ili atengeneze maumbo ya bidhaa anazotaka kwa ajili ya mapambo.

Chanzo: mwananchi.co.tz