Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malipo mradi wa maji Holili yamshtua kiongozi mbio za Mwenge

Kiongozi Mbio Za Mwenge Malipo mradi wa maji Holili yamshtua kiongozi mbio za Mwenge

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amehoji sababu ya malipo ya Sh299 milioni kwa mkandarasi aliyetekeleza mradi wa uboreshaji wa maji katika Mji wa Holili mkoani Kilimanjaro badala ya Sh188 milioni.

Pia, ameitaka Malamka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowasa) kukabidhi nyaraka zinazoonyesha malipo hayo yalivyofanyika.

Mradi huo unaohusisha ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 300, 000 unatarajiwa kunufaisha wananchi wa mji wa Holili wapatao 9, 705 na kuongeza usambazaji wa maji wa lita 690,000 kutoka mara moja hadi mara mbili kwa wiki.

Akizungumza leo Aprili 6, 2024 baada ya kukagua mradi huo wa maji, kiongozi huyo amesema ameshtushwa na malipo hayo, akihoji majibu ya wanaosimamia mradi huo kuwa, mkandarasi amelipwa fedha hizo kwa kuunganishiwa na malipo ya mradi mwingine anaotekeleza wilayani humo.

"Kwanza, mradi huu ulikuwa unaelekeza kujenga tenki la maji lenye lita za ujazo 300,000 lakini wakati wa ukaguzi wa nyaraka baadhi ya mambo tumeyabaini, wenyewe wali-'rise certificate' ya Sh188 milioni lakini malipo yaliyofanyika ni ya Sh299 milioni jambo ambalo kidogo limetushtua,” amesema Mnzava.

"Pili, tumeuliza wanasema ni kwa sababu yale malipo yaliyofanyika mkandarasi ana miradi zaidi ya mmoja na kwa sababu yeye ni mmoja ameunganishiwa malipo ya miradi yote miwili lakini kwenye usimamizi wa miradi tunafahamu kila mradi ni lazima ujitegemee."

Pia, Mnzava amehoji sababu ya mkandarasi huyo kukatwa kodi ya zuio la asilimia 5 kwa malipo ya Sh188 milioni badala ya Sh299 milioni ya fedha ambazo amelipwa mkandarasi huyo.

"Pia, kwenye hiyo Sh9 milioni, 'Certificate ya TRA registration (cheti cha usajili cha Mamlaka ya Mapato Tanzania) wa hayo malipo ipo Sh5 milioni, Sh4 milioni hatujaiona, kwa hiyo tumeelekeza waende wakatuletee hizo nyaraka tujiridhishe zaidi ilikuwaje kutoka Sh188 milioni kwenda kuwa Sh299 milioni," amesema Mnzava.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Ofisa Huduma kwa Wateja, Selestine Mtenga amesema utekelezaji huo wa uboreshaji wa huduma kwa maji katika mji wa Holili unatokana na changamoto kubwa ya maji iliyopo mjini hapo.

Amesema mahitaji ya maji katika eneo hilo ni lita 1, 700, 000 kwa siku, awali usambazaji wa maji ulikuwa lita 600, 000 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa maji wa lita 1,100,000 kwa siku.

"Rombowasa ilisanifu mradi huu wa maji mserereko kama jitihada ya kupunguza upungufu huo, lita 690, 000 zitaongezeka kwa siku, hivyo kupunguza upungufu uliokuwapo kwa asilimia 63," amesema Mtenga.

Chanzo: Mwananchi