Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malima atoa wiki 3  agizo la Majaliwa

9730886e1084dd8b50323612aa88375a.jpeg Malima atoa wiki 3  agizo la Majaliwa

Wed, 26 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ametoa wiki tatu kwa halmashauri za mkoa huo zitekeleze agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kukamilisha upandaji vitalu vya mkonge kwa ajili ya kugawa miche kwa wananchi.

Malima alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kujitambulisha kwa watendaji wa halmashauri na wakuu wa sekta mbalimbali zikiwezo za serikali na binafsi mkoani humo.

Alisema hajaridhishwa na kasi ya uanzishwaji wa vitalu katika halmashauri hizo zikiwamo ambazo bado hazijaanza kusafisha maeneo kwa ajili ya kupanda miche hiyo.

"Nimetembelea halmashauri zote lakini sijaridhishwa na kasi ya uwapo wa vitalu. Kuna wengine angalau wamefika ekari saba lakini kuna wengine hata kuanza kupanda bado, hili jambo sio la kuchekeana," alisema Malima.

Mkuu huyo wa mkoa alisema haiwezekani Waziri Mkuu atoe agizo halafu hadi sasa kuna kususua katika utekelezaji.

“Ikifika Juni 15 nitapita mwenyewe kwenye maeneo yote kuangalia namna ambavyo utekelezaji umefanyika. Tunataka Tanga baada ya miaka mitatu kutoka sasa tuweze kuzalisha tani 60,000 za mkonge, kama hatutaweka mikakati sasa ya kuhakikisha tunakuwa na mahitaji ya uhakika ni ndoto kufikia hilo lengo," alisema.

Malima alisema inaleta picha mbaya kwa mkoa wenye Bodi ya Mkonge na taasisi ya utafiti wa zao hilo kushindwa kufikia lengo la kuhakikisha vitalu vinakuwapo vya kutosha kwa ajili ya kuwapatia wananchi miche ya mkonge.

Aliziagiza kila halimashauri kuwa na mkakati wake ili kuona namna ambavyo serikali ya mkoa itakavyoweza kusaidia.

"Nia yangu ni kutoka uzalishaji wa tani 24,000 za mkonge hadi kufikia tani 60,000 ifikapo mwaka 2025 kwa mkoa huu pekee, hivyo ni lazima maofisa ugani mshirikiane ili kufikia lengo hilo,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Mazao (Tari) Mlingano, Dk Catherine Senkoro alisema changamoto kubwa iliyopo ni maofisa ugani kutokuwa na uelewa mzuri wa upandaji wa zao hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz