Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kero na usumbufu wanaoupata wakazi wa Makongo Juu kutokana na ubovu wa barabara mbioni kuwa historia.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Oktoba 30, 2019 Makonda amesema ujenzi wa barabara hiyo utaanza Novemba Mosi, 2019.
Hivi karibuni wakazi wa Makongo Juu walihojiwa na Mwananchi na kueleza adha wanayoipata kutokana na ubovu wa barabara hiyo, ikiwa ni pamoja na kuchelewa katika shughuli zao, magari kuharibika.
Barabara hiyo pia hutumiwa na wakazi wa Madale, Mbezi na Goba.
“Novemba Mosi tutazindua ujenzi wa barabara hii utakaogharimu Sh8.9 bilioni. Yale mateso na kero walizokuwa wakipata zitakuwa historia kwa sababu tunakwenda kuanza ujenzi nawaomba wawe wavumilivu,” amesema Makonda.