Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda kutumia Sh2.5 bilioni kujenga ofisi za CCM Dar

89254 Ccm+pic Makonda kutumia Sh2.5 bilioni kujenga ofisi za CCM Dar

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Kate Kamba amewataka wanachama kutafakari wamekifanyia nini chama hicho badala ya kusubiri chama kiwafanyie jambo.

Kamba ametoa rai hiyo leo Alhamisi Desemba 19, 2019 wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za CCM Wilaya ya Kinondoni.

Makonda anatarajia kutumia zaidi ya Sh2.5 bilioni kujenga ofisi za chama hicho katika Wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Temeke, Kigamboni, Ubungo, Ilala na Kinondoni.

"Kila mmoja ajiulize ameifanyia nini CCM? jiulize utafanya nini ili siku moja uje kukumbukwa ndani chama chako?" amesema Katekamba.

Amesema CCM sio chama cha matukio na hiyo ni sababu iliyowafanya washinde uchaguzi wa serikali za mtaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Awali,  Makonda amesema ujenzi wa ofisi hizo ni michango wake kwa chama hicho na hilo halina uhusiano wowote nafasi ya ubunge.

Katika maelezo yake, Makonda amesema, “wanaohoji kwamba fedha za Serikali zinatumika kujenga ofisi ya chama, wahoji kuhusu ofisi 73 za walimu zilizojengwa katika shule hapa Dar es Salaam, wahoji kuhusu watoto wanaopewa matibabu ya moyo na hospitali ya Chanika wahoji fedha zake zinatoka wapi.”

"Wapo wenye fikra potofu ambao wakiona ofisi hizi watadhani ubunge, nafasi hizi zipo kwa ratiba ya Mungu. Mkoa huu una majimbo mangapi?”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni amesema baadhi waliposikia Makonda ameahidi na ameamua kujenga ofisi hizo alihusianisha na uchaguzi wa mwaka 2020.

Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Zakaria Mwaisasu amewataka wanachama walioamua kukifanyia kazi chama chao wasiogope kelele ili mradi hawavunji kanuni na katiba ya chama hicho.

Chanzo: mwananchi.co.tz