Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku saba kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), kuziba viraka walivyochimba barabarani ili kuepusha madhara hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha.
Sambamba na hilo, ametoa tahadhari kwa wakazi wa jiji hilo wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi kuhama kabla athari za mvua hazijawakuta.
Amesema mkoa umeamua kutoa tahadhari mapema kwa kuwa mvua zitakazonyesha safari hii ni kubwa na kama hatua zisipochukuliwa zinaweza kuleta athari hasa kwa watu waishio maeneo hatarishi.
“Mamlaka ya Hali ya Hewa imeshatoa tahadhari kuwa mvua za safari hii zitakuwa kubwa sasa, nawasisitiza wananchi wachukue tahadhari, walio mabondeni na wanaishi kwenye nyumba zilizotitia wahame mapema.”
Amesema: “Kuhusu Tarura, nawapa siku saba wazibe viraka walivyoweka barabarani, haiwezekani wachimbe mashimo halafu yakae miezi miwili, mvua zimeanza yataleta madhara na kusababisha ajali.”