Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda atoa siku tano wenye picha za ngono kwenye simu kuzifuta

24807 Pic+ngono TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameunda kamati ya watu 15 kwa ajili ya kupambana na watu wanaojihusisha na biashara ya ngono, huku akiwataka walioweka picha za ngono katika simu kuzifuta kabla ya Novemba 5, 2018.

Akizungumza  na waandishi wa habari leo Jumatano Oktoba 31, 2018, Makonda amesema kuna mtandao wa watu wanaofanya biashara za ngono kwenye madanguro na kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo makundi ya Whatsapp, Facebook na Instagram.

Amesema kamati hiyo itakayoweka kambi eneo la Mburahati jijini hapa itajumuisha polisi, wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bodi ya Filamu, madaktari na wanasaikolojia.

"Kabla ya Jumatatu (Novemba 5, 2018) kila aliyeweka picha za ngono kwenye simu yake ajitahidi kufuta, nisingependa kuona kiongozi mtu mashuhuri unakamatwa. TCRA wanaweza kufuatilia mawasiliano kwa kiwango cha juu hata kwa miezi mitatu nyuma," amesema Makonda.

Makonda amesema kama biashara ya ngono itaachwa iendelee kufanywa inaweza kuhatarisha ustawi wa jamii.

"Mkoa wa Dar es Salaam ni kitovu cha maendeleo na hatuwezi kukwamishwa na watu wachache, tumetangaza vita na watu hawa," amesema.

Amesema kamati hiyo itaanza kufanya kazi Novemba 5 na tayari wameshapokea majina ya nyumba zinazotumika kurekodi video za ngono, biashara ya madanguro.

"Tungesema tufanye kimya na kujifanya jambo hili halipo ni kujidanganya. Jambo hili lipo na linaenda kinyume na maadili ya Kitanzania," amesema Makonda.

Chanzo: mwananchi.co.tz