Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda atoa mwongozo wa fursa wanafunzi vyuo vikuu

82780 Pic+makonda Makonda atoa mwongozo wa fursa wanafunzi vyuo vikuu

Tue, 5 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu kujitokeza kuomba nafasi za mafunzo kwa vitendo katika miradi mikubwa inayotekelezwa katika mkoa wake.

Makonda ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 3, 2019 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea miradi mbalimbali ukiwamo wa barabara ya mabasi yaendayo haraka wa Mbagala Mwisho - Kariakoo.

Amesema miradi hiyo imeanzishwa siyo tu kwa lengo la kuboresha miundombinu bali pia kuwapa fursa Watanzania hasa wanafunzi wa uhandisi kujifunza kwa vitendo.

"Wanafunzi wa vyuo vikuu jitokezeni kuomba field kwenye hii miradi. Sisi kama serikali tupo kuhakikisha kwamba tunawatengenezea mazingira mazuri ya kujifunza," amesema.

Makonda amewataka pia vijana wasio na ajira kwenda kuomba kazi kwa sababu serikali imewekeza zaidi ya Sh200 bilioni kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka pekee.

Amewataka vijana kuonyesha uaminifu wanapopewa ajira badala ya kuanza kuiba vitendea kazi na mali, jambo linalokwamisha miradi kukamilika kwa wakati mwafaka. Wakati akitembelea mradi wa barabara ya mwendokasi, Makonda amekutana na kundi la vijana wanaotafuta kazi na kumwomba awasaidie kupata kazi kwenye mradi huo.

"Sisi vijana wa Mbagala hatuna ajira lakini kwenye mradi huu kuna wafanyakazi wengi ambao hawatokei maeneo ya huku. Tunakuomba utusaidie na sisi tupate kazi," amesema Salum Risasi, mkazi wa Mbagala.

Makonda aliwataka vijana hao wajiorodheshe wote majina yao na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kuwapatia kazi kwa sababu wana moyo wa kufanya kazi licha ya kwamba leo ni Jumapili.

Chanzo: mwananchi.co.tz