Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Makomando’ kutumika kuokoa wajawazito, watoto

D5406f6ab4c06ee893d282710b900066 ‘Makomando’ kutumika kuokoa wajawazito, watoto

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, imeanzisha mfumo wa ushirikishaji ili kukabiliana na vifo vya akina mama, watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano.

Mfumo huo unashirikisha viongozi wa vijiji, kata, madiwani, viongozi wa mitaa na wananchi kuhusu namna ya kushiriki na kuzingatia elimu ya afya baada ya mwanamke kubainika ni mjamzito.

Mratibu wa huduma za afya uzazi na mtoto wilayani humo, Alexia Nonjela, alisema kutokana na changamoto ya vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano, idara ya afya wameanzisha mfumo uitwao UTURO Modal.

Alisema UTURO Modal ni mfumo waliouchukua katika Halmashauri ya Wilaya Mbarali, mkoani Mbeya baada ya kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kushirikisha jamii kuhakikisha wajawazito wote chini ya miezi mitatu wanaanza kuhudhuria kliniki kuepuka vifo.

Nnonjela alisema kupitia mpango huo, wanachaguliwa wanawake watatu maarufu kama (makomando) wanaojua kusoma na kuandika, wenye sifa za kujitolea, kuwa na siri, upendo na waaminifu, ambao hutoa elimu na taarifa za wanawake wanaopata ujauzito kuhakikisha wanahudhuria kliniki baada ya miezi mitatu ya mwanzo.

“Tulizindua huu mkakati mwezi Februari, mwaka huu na ndani ya muda mfupi tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa, ambapo kabla ya kuanza UTURO modal vifo vya akina mama kuanzia Januari mwaka huu mpaka kufika Machi tulikuwa na akina mama wengi waliofariki kutokana na matatizo ya uzazi,” alisema.

Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Adalberth Haule, alisema mfumo wa UTURO kutokana na matokeo mazuri ambayo yalipatikana Mbarali kwa kumaliza vifo vya akina mama na watoto ndani ya miaka 22, Wizara ya Afya iupo mbioni kuurasimisha nchi nzima.

"UTURO imeanza kuleta matokeo chanya kwani mwaka jana 2019 pekee, watoto wachanga 217 na wakina mama 15 walifariki, lakini sasa mabadiliko makubwa tunayaona ikilinganishwa na mwaka jana," alisema Haule.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi, Hanji Godiogodi, alisema mfumo huo utapunguza kwa kiasi kibwa vifo vya akina mama na watoto ambavyo kwa kiasi kikubwa vilikuwa vinatokea Mbozi hasa vijijini.

Chanzo: habarileo.co.tz