Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makinda avutiwa upanuzi chuo Hubert Kairuki

93e454221330a7c795bcb74fe46a0c78.jpeg Makinda avutiwa upanuzi chuo Hubert Kairuki

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SPIKA mstaafu, Anne Makinda amepongeza upanuzi unaofanywa na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) maeneo ya Boko, Dar es Salaam, kwani kitasaidia kutoa wahudumu wengi wa sekta ya afya nchini.

Makinda ambaye kwa sasa ni mkuu wa chuo hicho, aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na wafanyakazi, walimu na wanafunzi wa chuo hicho ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.

Alisema anakifahamu chuo hicho tangu kuanzishwa kwake kwani kimekuwa kikifanya vizuri kwa kutoa wahitimu ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye sekta ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nampongeza Makamu Mkuu wa chuo kwa kutoa wahitimu bora na ambao wana nidhamu, huwa nakutana nao maeneo mengi wanayofanya kazi unaona kabisa huyu daktari au muuguzi amefundishwa na akafundishika. Endeleeni kutoa huduma bora watu watawakimbilia,” alisema Makinda.

Aidha, alisema amesikia changamoto ya mikopo kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho ambayo alisema ataifikisha kwa wahusika ili ifanyiwe kazi wahudumiwe kama wengine.

“Mwenyekiti wa bodi aliwahi kuyasema haya mbele yangu kwamba wanafunzi hawa wakitoka hapa wanakwenda kufanyakazi kwenye hospitali za serikali sasa kwa nini wakose mikopo, mimi nimelielewa na nitalifikisha kwa wahusika,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu na Afya Kairuki (KHE), Kokushubira Kairuki aliiomba serikali isiwatoze fedha wanachuo wanapokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo kwani mwisho wa siku wanakwenda kulitumikia taifa.

“Tunapata shida wanafunzi wetu wanapokwenda kufanya mazoezi kwa vitendo kwani fedha wanazotaka ni kubwa nasisi hatuwezi kuwaongezea ada wanafunzi kufidia fedha hizo tunazotozwa hivyo tunaomba wasitutoze,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, John Ulanga alisema chuo kimeendelea kuongeza uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali na kuongeza walimu wenye weledi, hivyo kukifanya chuo kuendelea kuwa bora.

Alimpongeza Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone kwa kuimarisha ubora wa ufundishaji hali inayokifanya chuo kuendelea kuwa miongoni mwa vyuo vikuu bora duniani na kwamba ndiyo sababu kinapata wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz