Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makamu wa Rais kuzindua jengo la mabilioni Arusha

15191 Pic+makamu TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuwekeza katika jengo la kisasa la kituo cha Utalii Arusha, litakalozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Samia Suluhu Septemba 16, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Septemba 1, 2018 baada ya kutembelea jengo hilo lililojengwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Arusha, Gambo alisema Serikali imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo .

Gambo alisema, jengo hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Sh45 bilioni, litatoa huduma zote za utalii na hivyo kuondoa adha ya watalii kupata huduma mbali mbali katika jiji la Arusha.

"Arusha ndio kitovu cha utalii, hivyo ujenzi wa jengo hili unaendana na hadhi ya Arusha lakini pia ni moja ya vitega uchumi vya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro tofauti na kutegemea watalii kutembelea hifadhi hiyo," alisema.

Alisema Serikali pia inaridhishwa na ongezeko la mapato katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo mwaka 2016/17 walipata Sh102 bilioni, 2017/18 Sh124 bilioni na mwaka 2018/19 zinatarajiwa kupatikana Sh156 bilioni.

"Ongezeko la mapato haya ni ishara mnamuelewa Rais wetu John Magufuli katika suala zima la kuongeza mapato ya Serikali," alisema

Awali, mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Profesa Abiud Kaswamila, alisema jengo hilo litazinduliwa rasmi Septemba 16 na Makamu wa Rais Samia Suluhu.

Alisema jengo hilo linakidhi viwango vya kimataifa na litakuwa na sehemu ya kuegesha magari chini, jambo ambalo linaondoa tatizo la kukosekana sehemu ya maegesho ya magari.

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk Fred Manongi alisema hadi sasa jengo hilo, limegharimu kiasi cha Sh39.6 bilioni na hadi kukamilika litagharimu Sh45 bilioni ambazo zitarudi katika kipindi kisichozidi miaka 10.

Meneja uwekezaji wa Ngorongoro, Needpeace Wambuya, alisema hadi sasa asilimia 45 ya jengo imepata wapangaji na inakadiriwa mapato ya kodi kwa mwezi yatakuwa Sh 366 milioni na hivyo ndani ya miaka 10 gharama za ujenzi zitakuwa zimerudi.

Msanifu wa jengo hilo, mkurugenzi wa taasisi ya Afri- Arch Associates, Profesa Camilius Lekule alisema jengo hilo limejengwa kisasa kabisa na kwa kuzingatia sura ya Creta ya Ngorongoro na nyumba za asili za kimasai.

Chanzo: mwananchi.co.tz