Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makalla awatuliza wafanyabiashara Kariakoo

31a6555bfe6e1c11a68097ac73152584.jpeg RC Makalla

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ametanzua sintofahamu ya wafanyabiashara wa soko la mzunguko, soko la wazi na wenye vibanda kuzunguka Soko Kuu la Kariakoo waliopinga kuhamishwa huku wenzao wa soko dogo wakitakiwa kubaki kuendelea na biashara.

HabariLEO imeshuhudia jana asubuhi wafanyabiashara hao wakiitaka serikali kutoa uamuzi wa ama kuwaondoa wote au kuwabakiza wote na siyo wengine waondolewe na wengine wabaki kwa kuwa kama ni athari ya moto imewaathiri wote.

“Watu tuna mikopo, tunasomesha watoto, kama ni moto umetuathiri wafanyabiashara wote, sasa kwa nini wenzetu wa soko dogo waambiwe wabaki halafu sisi wengine wa soko la mzunguko na soko la wazi tuambiwe tuondoke tuhamie Soko la Kisutu na Soko la Machinga, tunataka ama wote tuondolewe au wote tubaki,” walisema wafanyabiashara Eli Kaaya na Mwanaidi Athumani wanaouza mboga na matunda.

Katibu wa Soko la Wazi, Sudi Jongo aliunga mkono kauli ya wafanyabiashara hao kwamba kama ni janga la moto limewaathiri wote, hivyo kama ni kupisha ukarabati na uchunguzi, ingefaa wote waondolewe na siyo wengine wabaki.

Mfanyabiashara mwingine, Jumanne Zabibu aliiomba serikali iwaruhusu kutoa bidhaa zao kwenye soko la shimoni kwani nyingi ni bidhaa za kuharibika haraka.

Kutokana na sintofahamu hiyo, ndipo Makalla alifika sokoni hapo na kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara wa soko la wazi, soko la mzunguko, soko dogo, wafanyabiashara wa vigoli na viongozi wa Machinga na kukubaliana kwamba waondoke kwa kuwa maeneo hayo siyo salama, pia wapishe uchunguzi na ukarabati wa soko.

“Sisi kama serikali jukumu letu ni kuhakikisha usalama wenu, hatupo hapa kumuonea mtu yeyote, ndiyo maana tunawataka kabla ya kuondoka hapa kila mmoja ajiorodheshe jina lake, namba yake ya simu, biashara aliyokuwa anafanya, ili ukarabati wa soko ukikamilika, kila mfanyabiashara arudi hapa kwenye eneo lake,” alisema Makalla.

Kuhusu wafanyabiashara wa shimoni wanaofikia 397, nao aliwataka wajiorodheshe ili watakaporuhusiwa kuingia baada ya miundombinu ya umeme na feni kurekebishwa iwe rahisi kuwatambua.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija aliwataka viongozi wa wafanyabiashara hao kuhakikisha kila mfanyabiashara anajiorodhesha jina lake, mtaji wa biashara yake na hasara aliyopata ili taarifa hizo ziisaidie serikali kujua kiwango cha hasara kilichosababishwa na moto huo.

Makamu Mwenyekiti wa Machinga katika Soko la Kariakoo, Namoto Yusuph Namoto, alisema kwa kuwa Soko Kuu la Kariakoo linagusa maisha ya wafanyabiashara wengi wadogo, moto huo umeathiri maisha yao kwa kiasi kikubwa.

Katibu wa Wafanyabiashara ya Vigoli, Anna Mzena alimuomba mkuu wa mkoa awahakikishie kimaandishi kama kweli ukarabati utakapokamilika watarejeshwa sokoni hapo. Akijibu hoja hiyo, Makalla alisema tamko lake kwamba watarudi hapo ni ya uhakika hivyo wasiwe na mashaka.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah amewapa pole wana Dar es Salaam na Watanzania wote kwa janga la moto katika Soko Kuu la Kariakoo.

Amesema wananchi wa Zanzibar wanawapa pole.

Aidha, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na timu yake kwa kazi kubwa wanayofanya na kuhakikisha shughuli za kibiashara zinaendelea kwa utulivu na amani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz