Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makalla amchana Lema, ataka wanawake wampuuze

RC Makallaa Makalla amchana Lema, ataka wanawake wampuuze

Thu, 9 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amewataka wanawake kupuuzia kauli aliyoitoa aliyewahi kuwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema kwamba benki za vijijini (Vicoba) ni umasikini.

Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano na chombo kimojawapo cha habari, Lema aliyerejea nchini Machi Mosi akitokea nchini Canada alikokimbilia tangu mwaka 2020 na familia yake, amekaririwa akisema Vicoba ni umasiki na ndio maana alimwondoa mkewe kwenye benki hizo.

Akizungumza jana Machi 8, katika maadhimisho ya siku wanawake Mkoa wa Dar es Salaam, Makalla ambaye alikua mgeni rasmi amesema Mamlaka za udhibiti zitoe ushirikiano kwa wanawake katika ujasiliamali ambao wanafanya.

"Huyu anayepiga vita Vikoba hana njaa, huyo hajui shida za wanawake wa Tanzania.

"Kuna watu wamefanikiwa kwa kuanza kwa kitu kidogo, huwezi kuanza na vitu vikubwa, msikatishwe tamaa," aliongeza Makalla.

Pia amezitaka mamlaka za udhibiti wa viwango vya bidhaa kuwatia moyo wanawake wajasiliamali badala ya kuwakatisha tamaa ili kufikia ndoto zao.

"Nikiwa hapa nimeona taasisi mbalimbali ikiwepo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na nyingine, nitoe wito, watieni moyo wanawake msiwakatishe tamaa," amesema Makalla.

Pia Makalla amewataka wananchi kununua bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wajasiriamali ili kukuza pato lao na Taifa kwa ujumla.

"Niwaombe wanawake wajasiriamali kuzingatia ubora katika bidhaa zao ili kukidhi ushindani katika soko la kitaifa na kimataifa," amesema.

Naye Ofisa Elimu mwandamizi wa Makumbusho ya Taifa, Anamery Bagenyi, amesema Katika kuunga mkono juhudi za serikali kukuza na kuwawezesha wajasiriamali wadogo, Makumbusho ya Taifa imetenga eneo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo.

"Wajasiriamali wadogo tumewatengea eneo ambapo wanalipia kodi kidogo na wanapata nafasi ya kuuza bidhaa zao kwa watalii wa ndani na nje wanaotembelea vituo vya Makumbusho ya Taifa na Malikale," amesema Anamary.

Wanawake wafanyakazi katika Makumbusho ya Taifa wamefanya ziara kutembelea maeneo mbalimbali ya kiutalii jijini hapa ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Utalii ambao umekua ikihamasishwa na serikali.

Naye Mlezi wa Majukwaa ya wanawake mkoa wa Dar es Salaam, Devota Likokolo amesema wanawake wanaishukuru serikali kwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha Likokolo ameiomba serikali kuwasaidia wanawake kupata elimu ya mafunzo ya vitendo katika fani mbalimbali ikiwemo uongozi na Ujasiriamali.

"Elimu ya malezi na makuzi iendelee kitolewa kwa jamii ili watoto na vizazi vijavyo viwe na tabia njema," ameongeza Likokolo.

Chanzo: mwanachidigital