Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makalla aanika athari za kujenga bila Hatimiliki

Makalla6 Amos Makalla, RC DSM

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Athari za kujenga nyumba bila hatimiliki baada ya kuvamia maeneo ya watu wengine zimeanza kujitokea wazi.

Hii ni baada ya migogoro ya ardhi kuendelea kushika kasi nchini na baadhi ya nyumba kuanza kubomolewa.

Ni katika mazingira hayo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka wananchi waliovamia maeneo yasiyo yao jijini humo kuondoka wenyewe mara moja.

Makalla ametoa agizo hilo ikiwa ni siku chache tangu nyumba zaidi ya 400 kubomolewa eneo la Mabwepande jijini humo kutokana na kujenga maeneo ya Serikali.

Aidha, nyumba zaidi ya 50 zilibomolewa wiki iliyopita Mpigi Magoe Wilaya ya Ubungo kutokana na kujengwa katika eneo la mtu binafsi.

Kufuatia matukio hayo, mkuu huyo wa mkoa jana alikutana na watendaji wa mkoa huo kuzungumzia masuala mbalimbali likiwemo la kukithiri kwa migogoro ya ardhi, ambalo alisema ni moja ya kero kubwa alizokutana nazo alipofanya ziara katika majimbo matano ya mkoa huo.

Advertisement Alitaja maeneo yaliyokithiri kwa vitendo hivyo kuwa ni wilaya ya Kinondoni maeneo ya Goba, Mabwepande na hata Serikali ilipotumia busara kuwamilikisha baadhi ya maeneo kwa kuyalipia ili kuleta amani, wameonekana sasa wamejenga utamaduni wa uvamizi wakijua itawaonea huruma.

“Hilo limefanyika eneo la Wazo ambako kulikuwa na wavamizi zaidi ya 4,000 kwenye kiwanja ambacho ni mali ya kiwanda cha saruji cha Wazo.

“Mnaposikia Chasimba, Chatembo wamevamia tu eneo la Wazo wakaanza kujenga, wameshindwa kesi mahali kote, huruma ikaja walipie, nafurahi kwamba wameendelea kwa kasi kulipia na mtu ambaye hatalipia, huyo aondoke yeye mwenyewe maana kashashindwa mwenyewe,” alisema.

Akisisitiza hilo, Makalla alisema, “huwezi ukachukua haki ya mwenzako na ndio maana kuna sheria na taratibu za kumiliki ardhi, wavamizi kokote mlipo kazi imeanza, popote mlipo nipo ‘live’, umevamia ardhi, umevamia kiwanja cha mwenzako, unakaa tu hapo nakuomba, sitaki kukuona, hakuna mtu atabaki salama.”

Katika maelekezo yake, Makalla alizitaka mamlaka za serikali za mitaa zisiwe sehemu za usimamizi wa uuzaji holela ardhi zinazoleta matatizo.

Baada ya agizo, gazeti hili lilizungumza na Kamshina wa Ardhi mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kahyera kujua undani wa migogoro hiyo na idadi yake, akasema zaidi ya wakazi 20,000 wamevamia maeneo jijini humo.

Alitaja baadhi ya maeneo na idadi ya wavamizi kuwa ni Somji 478, Nyakasangwe 6,439, Chasimba 4,070, Mabwepande 9,140 na waliovamia eneo lililopimwa la Mbweni Mpiji ni 278.

Hali hiyo si kwa Dar es Salaam pekee, huko Dodoma, mkuu wa mkoa Anthony Mtaka naye alizungumzia migogoro ya ardhi hivi karibuni akisema Jiji la Dodoma linaloongoza nchi nzima, akitaja kipindi cha 2020/21 kuwa ililipotiwa migogoro karibu 9,000 na hadi mwishoni mwa wiki iliyopita zaidi ya migogoro 1,900 haijaanza kutatuliwa.

Mei 26 mwaka huu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akiwasilisha bajeti ya 2022/23 ya wizara yake alisema moja ya shughuli za wizara kwa mwaka huu ni kutatua migogoro ya ardhi.

Matatizo hayo yamesababisha wizara hiyo kuwahamisha baadhi ya watumishi, wengine kuwasimamisha kazi na wawili kutokana na kusababisha migogoro ya ardhi.

Jiepushe ni migogoro

Akizungunzia namna ya kujiepusha na migogoro huyo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Allan Kijazi alishauri kila mtu kujiridhisha na uhalalai kabla ya kununua ardhi.

“Inabidi wajenge tabia ya kujiridhisha kupitia ofisi za halmashauri ya mkoa au wilaya ili kujua eneo limetengwa kwa ajili ya matumizi gani,” alisema Dk Kijazi.

Alisema Serikali hutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo viwanda, huduma za jamii, ni vyema mnunuzi kufuatilia matumizi sahihi ya eneo husika.

“Kama ni la makazi ajiridhishe kama kuna umiliki au hakuna umiliki uliotolewa na Serikali kwa eneo hilo baada ya hapo ndiyo aendelee na taratibu za manunuzi na ujenzi,” alisema

Dk Kijazi alibainisha kuwa wanunuzi wa sasa hawafuatilii kujua umiliki wa maeneo hayo au yametengwa kwa ajili ya shughuli gani, jambo ambalo limekuwa likifanya migogoro ya ardhi kuendelea na watu kupata hasara.

“Lakini linapotokea tatizo ndiyo utawaona wao ofisi za ardhi kuleta malalamiko bila kujua wangetumia ofisi hiyohiyo tangu mwanzo hayo yasingekuwepo,” alisema Dk Kijazi.

Kuhusu matumizi ya Serikali za mitaa katika ununuzi wa viwanja, alisema viongozi wa maeneo hayo wanapaswa kusimamia matumizi yake vyema na kuhakikisha wanawaelekeza wananchi kufuata taratibu zilizowekwa.

“Tunazo taarifa za baadhi ya wenyeviti na watendaji (wa mitaa)ambao wamekuwa wakikiuka taratibu za umiliki wa ardhi na kujihusisha na vitendo vya rushwa. Wanapobainika wamehusika huwa wanachukuliwa hatua za kisheria na vyombo husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live