Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makalla: Serikali haiwezi kuwafanyia kila kitu

Makalla 1 Amos Makalla, RC DSM

Wed, 16 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amewaasa wakazi wa wilaya ya Ubungo kuacha kuwaza kila kitu kitafanywa na Serikali badala yake katika baadhi ya mambo wanatakiwa kufanya wenyewe kwa kushirikiana na wadau kutoka sekta binafsi.

Hayo ameyasema jana Jumanne Novemba 15, 2022 baada ya kuzindua Hotel iliyopo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam.

Makalla amesema amefarijika kuona uwekezaji mzuri uliofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kufanikisha ujenzi wa hoteli hiyo.

"Nina wapongeza sana Halmashauri ya manispaa ya Ubungo kwa kufanya uamuzi wa kushirikiana na mwekezaji kutoka sekta binafsi katika kufanikisha jambo hili," amesema.

Kadhalika Makalla amesema ameona hoteli inapendeza kwa kuwa safi na yenye kuvutia hivyo usafi alioukuta leo uwe wa kudumu.

"Biashara inataka nidhamu, huduma bora na usafi bila kusahau ubunifu uliotukuka, hivyo haya mnatakiwa kuyazingatia," amesema.

Hata hivyo, Makalll amewaeleza Halmashauri ya Ubungo pamoja na mwekezaji kwa yale waliyokubaliana baina ya pande mbili wanatakiwa kuyatekeleza vizuri na kwa uwazi.

Naye Meya wa Halmashauri ya Ubungo, Jaffary Nyaigesha amesema wao kama Halmashauri watahakikisha wanafanya mabadiliko katika kituo hicho kwa kuifanya kuwa bora na ya kimataifa.

"Tutahakikisha tunaitoa stendi kwenye hali ya uswazi na kuwa kituo cha kimataifa," amesema

Kwa upande wake, kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubongo, Dk Peter Nsanya wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa hoteli hiyo amesema Watanzania watakaotumia stendi hiyo ya magufuli watapata nafasi ya kupumzika katika hoteli hiyo kwa bei nafuu ya kitanzania.

Dk Nsanya alimwaga sifa kwa mwekezaji Benjamini Fredy ambaye pia ni mkazi wa kimara kutoka wilaya ya Ubungo.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James amesema halmashauri yake imehakikisha Dar es Salaam inakuwa na mapato ya kutosha ili mapato hayo yakasukume maendeleo kwa wananchi hivyo Halmashauri ikaja na ubunifu wa kutumia stendi ya magufuli kwa ajili ya kujipatia mapato.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live