Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makalla: Msiruhusu watoto walale na wageni

B6ccdaed2d9b6619da10fc15d1c80d56.jpeg Makalla: Msiruhusu watoto walale na wageni

Fri, 28 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amezishauri familia zisiruhusu watoto walale chumba kimoja na wageni wanaowatembelea au ndugu wanaoishi nao.

Makalla alitoa ushauri huo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kuweka mkakati wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa watoto mkoani humo.

Mkutano huo uliandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) na kuwakutanisha watendaji wa ofisi hiyo wakiwemo madaktari, ustawi wa jamii, dawati la jinsia, wanasheria, wakuu wa wilaya, wanasaikolojia na watendaji wengine.

“Niwatake wananchi kuanzia ngazi ya familia kuacha tabia ya kulaza watoto chumba kimoja na wageni wanaotembelea nyumbani au ndugu waishio hapo kwa sababu vitendo vya ukatili

kwa watoto vimebainika kufanywa na ndugu wa karibu.” “Inashauriwa kama wewe una watoto wako hata kama mgeni wako ni anko wao usimwamini alale na watoto, maana matukio mengine yamefanywa na ndugu wa karibu, usiruhusu na mimi nasema usiruhusu mgeni au ndugu wa hapo nyumbani alale na watoto,” alisema Makalla.

Mkuu huyo wa mkoa alisema watoto wengi waliofanyiwa ukatili wamefanyiwa na ndugu wa karibu wakiwemo wajomba, binamu, babu, baba mdogo ambao wanaishi au wamezitembelea familia hizo.

Kwa mujibu wa Makalla, baada ya wahusika kufanya vitendo hivyo huwatisha watoto wasiseme hivyo watoto wengi wameharibika pia kisaikolojia kwa kuwa wanaendelea kuvumilia vitisho hivyo.

“Hadi siku wazazi wakibaini mtoto ameshaharibika na hapo ameharibika kimwili lakini pia kisaikolojia, kwa maana aliyemfanyia ukatili awe anko, binamu, baba mdogo au ndugu mwingine wa familia anamtisha,” alisema.

Alisema kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu yalifunguliwa mashauri 1,243 katika wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam na katika ngazi ya halmashauri yamefunguliwa 991 yanayohusiana na ukatili kwa watoto na ukatili kwa wanawake yalifunguliwa mashauri 991.

“Mashauri na taarifa za ukatili ni nyingi kwa kipindi cha miezi mitatu tu, kesi ni nyingi na matukio ya ukatili Dar es Salaam yanatisha,

mengi yameshafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Makalla.

Mkurugenzi Mkuu wa WiLDAF, Anna Kulaya alisema kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia mkoani Dar e Salaam kuanzia ngazi ya familia, jamii na maeneo ya kazi.

“Ukatili ni mkubwa, ripoti na tafiti nyingi zinaonesha wanaoathirika zaidi ni watoto na wanawake, japo wapo pia wanaume wanafanyiwa ukatili lakini sio wengi ikilinganishwa na makundi hayo,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz