Wakazi wa kata ya Tandika Manispaa ya Mtwara Mikindani wameiomba Serikali kuwasaidia kusafisha eneo la Makaburi Msafa ili kudhibiti vitendo vya wizi pamoja na watu kugeuza eneo hilo kuwa sehemu ya kufanyia mapenzi wakati wa usiku.
Akizungumza mtaani hapo, Zamda Meza mkazi wa Tandika amesema licha ya kuwa na kipori ambacho hugeuzwa ‘gesti bubu’ lakini kumekuwa na vibaka ambao hutumia eneo hilo na kusababisha watu kushindwa kupita usiku.
“Hili eneo la makaburi lina majani mengi ambayo yanatunza watu wabaya hivyo kuwa tishio kwa wanawake na watoto hasa wakati wa usiku yaani eneo hili makaburi hayaheshimiki watu wemegeuza ‘gesti bubu’ afadhali uwekwe utaratibu wa kufanya usafi wa mara kwa mara” amesema Zamda.
Nae Zailati Yusuph mkazi wa eneo hilo amesema licha ya majani marefu na watu kulitumia vibaya eneo hilo kuligeuza nyumba ya kulala wageni pia ni kubwa hivyo usafi wake unashindwa kufanyika.
“Makaburi msafa ni eneo chafu watu wanalitumia vibaya sana vibaka wanakaa hapo wanapita katika nyumba wanaiba wanakimbilia kujificha hapo, wengine wanatumia kama gesti wakati wa usiku hasa ukizingatia mazingira yenyewe yana vichaka,”amesema Zailati.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Thomas Chonde amesema kuwa kutokana na ukubwa wa eneo hilo usafi unaofanyika umekuwa sio wa kuridhisha licha ya wananchi kujitoa na kufanya usafi.
“Kwa muda mrefu nilikuwa nawashauri wananchi na kuwashawishi kufanya usafi wa mara kwa mara ili kuondoa vichaka katika makaburi, lakini hapa tumekuta watu wanaiba vitu huko wanakuja kugawana hapa, wengine wanatumia kufanyia mapenzi hapa, amesema.
kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tandika, Haruni Selemani amesema katika eneo hilo hali imekuwa mbaya, eneo limekuwa chafu pia ni kubwa hata ukitoa wito wa kusafisha wanaojitoa ni wachache kwaajili ya kufanya usafi.